13 September 2012

Bao la Okwi lamgusa Milovan


Na Mwandishi Wetu

BAO la kusawazisha lililofungwa na mshambuliaji, Emmanuel Okwi wa Simba limemkuna kocha wa timu hiyo, Milovan Cirkovic kwa madai kwamba hakutarajia kama mchezaji huyo angefunga bao akiwa katika mazingira magumu.


Okwi alifunga bao la pili katika mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC, dakika ya 68 kwa shuti la mguu wa kushoto mbele ya mabeki Aggrey Morris na Said Morald, katika mechi iliyochezwa juzi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza mara baada ya mechi hiyo kumalizika, Milovan alisema mechi hiyo ilikuwa ngumu kwao na hakutarajia kama vijana wake wangetoka nyuma kwa mabao 2-0 na kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 na kutwaa Ngao ya Jamii.

"Matokeo yamenishangaza sana, kweli Simba ni timu kubwa kwani sikutarajia kupata matokeo kama yale kwa jinsi Azam ilivyokuwa ikicheza, Okwi alifunga bao la kusawazisha katika mazingira ambayo sikudhani kama atafunga," alisema Milovan.

Alisema kipindi cha kwanza Azama walicheza vizuri na mbaya zaidi bao la mapema, ndilo lililomchanganya na kumfanya aumize kichwa zaidi, lakini pamoja na kushinda anaipongeza Azam kwa kiwango walichokionesha.

Akizungumzia mabeki wake kuruhusu mabao mengi, Milovan alisema: "Tunachoangalia kwa sasa ni kwenda mbele na si kuangalia tulipotoka, bado naendelea kuijenga timu yangu katika safu ya ulinzi na ndiyo maana ninachezesha wachezaji tofauti tofauti.

Alisema kutokana na mechi walizocheza hadi sasa ameshapata safu ya ulinzi aliyokuwa akiitaka na yupo tayari kutetea ubingwa wa ligi hiyo, ambayo mechi itaanza mwishoni mwa wiki.

Katika mechi hiyo, Milovan alilazimika kumuingiza beki Juma Nyosso kuchukua nafasi ya Pascal Ochieng, ambaye mashabiki wa timu hiyo hawakuridhishwa na kiwango chake kwani alishindwa kuwakaba John Bocco 'Adebayor' na Kipre Tchetche, ambao katika kipindi cha kwanza walikuwa mwiba kwa Simba.

Lakini kuingia kwa Nyosso, kuliifanya safu ya ulinzi ya Simba kuimarika ambapo mashambulizi mengi yaliyokuwa yakipelekwa beki huyo aliyaondosha na kuwafanya maelfu ya mashabiki wa timu hiyo kumshangilia kila anapogusa mpira.

No comments:

Post a Comment