13 September 2012
Saintfeit apiga mkwara mzito Yanga *Kijiko, Nurdin kuikosa Prisons
Na Zahoro Mlanzi
KOCHA Mkuu wa Yanga, Tom Saintfeit amewataka wachezaji wake kuhakikisha wanashinda kila mechi na kuwahadharisha hakuna timu ndogo katika Ligi Kuu Bara, kwani hataki kuona wamefungwa.
Timu hiyo inatarajiwa kuondoka leo saa 5.30 asubuhi kwa basi ikiwa na wachezaji 22 na viongozi wa benchi la ufundi watano kwenda Mbeya, huku ikiwabakisha jijini Dar es Salaam nyota Juma Seif 'Kijiko', Nurdin Bakari, Ladslaus Mbogo na Idrisa Rashid.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Saintfeit alisema mechi ya Jumamosi dhidi ya Prisons itakuwa na ushindani, hivyo amewataka wachezaji wake kuhakikisha hawapotezi mchezo huo.
"Prisons ilishika namba mbili miongoni mwa timu zilizopanda daraja na watakuwa na mashabiki wao kwa kuwa tunacheza kwenye uwanja wao, wakifungwa hawana la kupoteza lakini tukifungwa itakuwa ni miujiza kwao na tukitoka sare watashangilia pia," alisema Saintfeit.
Alisema wanatakiwa kuwa makini katika mechi hiyo kwani inaonekana msimu uliopita, walipoteza pointi 21 kwa mechi za ugenini na pointi nane za nyumbani, hivyo hapendi kuona kitu kama hicho kinajirudia tena msimu huu.
Kocha huyo alisema kikosi chake kipo vizuri na hawana mchezaji yeyote mwenye majeraha, lakini ameamua kuondoka na wachezaji 22 kutokana na mahitaji ya mechi yenyewe na si kama waliobaki hawana uwezo.
Aliwataja wachezaji wanaondoka leo ni makipa Yaw Berko na Ali Mustapha 'Barthez', mabeki ni Shadrack Nsajigwa, Juma Abdul, Godfrey Taita, Mbuyu Twite, Kelvin Yondani, Nadir Haroub 'Canavaro', David Luhende, Oscar Joshua na Stephano Mwasika.
Viungo ni Athuman Idd 'Chuji', Haruna Niyonzima, Frank Domayo, Rashid Gumbo, Nizar Khalfan, Shamte Ally na Simon Msuva na washambuliaji ni Jeryson Tegete, Didier Kavumbagu, Said Bahanunzi na Hamis Kiiza 'Diego'.
Wengine ambao aliwaacha tofauti na wale wanne ni Salum Telela, Said Mohamed, Omega Seme na Issa wa timu ya vijana (U-20).
Aliongeza kuwa wachezaji walioondoka na timu amewachagua kulingana na nidhamu, uwezo, mechi za kirafiki na sababu za kiufundi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment