05 September 2012
Azam yaipania Simba Ngao ya Jamii
Na Mwandishi Wetu
KLABU ya Azam FC, imetamba kwamba itaendeleza rekodi ya kutofungwa na Simba, katika mechi zake na kwa kuanza itaanza katika Ngao ya Jamii itakayochezwa Jumanne Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Jaffar Idd alisema timu yake inaendelea vizuri na mazoezi na inajipanga kwa mechi ya Ngao ya Jamii na Ligi Kuu Bara.
Alisema wanacheza mechi nyingi za kirafiki ili kuhakikisha kocha wao mpya, Bunjak Boris anapata wachezaji wa kikosi cha kwanza ambao wataifanya timu hiyo izidi kufanya vizuri katika ligi.
"Tumecheza na Coastal Union na JKT Oljoro na zote tumeshinda, bado tunahitaji mechi zaidi kwa ajili ya kujiweka sawa kabla ya kucheza na Simba Jumanne, tuna imani tutaendeleza wimbi la ushindi katika mchezo huo," alitamba Idd.
Alisema wanajua wapinzani wao ni timu kongwe nchini, lakini soka la sasa lina mageuzi makubwa ikilinganishwa na miaka ya 1970, hivyo kikubwa ni kujiandaa vizuri ili kuongeza ushindani zaidi.
Msemaji huyo alisema mechi hiyo itakuwa ya aina yake kutokana na timu zote kufanya usajili mzuri na pia zinaundwa na wachezaji vijana, huku kila moja ikicheza mechi nyingi za kirafiki.
Alisema kwa sasa timu yake inatafuta mchezo mmoja wa kirafiki kabla ya kucheza na Simba, ikiwa ni muendelezo wa maandalizi ya ligi hiyo.
Timu hizo kwa mara ya mwisho zilikutana katika Kombe la Kagame hatua ya robo fainali ambapo, Azam iliichapa Simba kwa mabao 3-0.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment