07 August 2012
Watanzania watakiwa kuwa na moyo wa kusaidiana
Na Mwandishi wetu, Arusha
WATANZANIA wametakiwa kuimarisha utamaduni wa kusaidiana kama njia ya kujenga umoja miongoni mwao na kufikia maendeleo wanayoyataka.
Changamoto hiyo ilitolewa na Bw. Emmanuel Ole Naiko aliyekuwa mgeni rasmi wakati wa harambee ya ujenzi wa kanisa la KKKT Usharika wa Moivaro Arusha mwishoni mwa wiki jijini humo.
Zaidi ya Tshs 31 milioni zilikusanywa katika harambee hiyo ikiwa ni pesa taslimu na ahadi kutoka kwa washarika na watu mbalimbali.
"Nimefarijika sana kwa kunipa heshima kubwa kuniomba niwe mgeni rasmi katika shughuli hii,mmenithamini sana, hivyo nawaomba muendelee na moyo wakujitolea katika kujenga nyumba za ibada na taifa letu kwa ujumla, " alisema Bw.Ole Naiko.
Alisema Watanzania ni watu ambao hawana mali nyingi lakini wamekuwa mstari wa mbele katika kumtolea Mungu, akisema hiyo ni imani kubwa ambayo haina budi kuendelezwa na kurithishwa vizazi vijavyo.
"Nimejifunza jambo moja kubwa sana kwenu, na hili litakuwa kama kioo na mwongozo kwangu, watanzani ni watu ambao hawana mali nyingi za kutisha wanaishi katika maisha ya kawaida lakini katika sula la imani mmekuwa mkijitoa sana, hili ni jambo jema,"aliongeza.
Akinukuu mifano mbalimbali kutoka katika biblia, Bw.Ole Naiko alisema ni vema watu wakamtanguliza Mungu kwanza katika kila jambo wanalolifanya ili waweze kufanikiwa katika shughuli zao wanazozifanya.
Aidha alitoa shukrani zake za dhati kwa Askofu Thomas Laiser ambaye ni mkuu wa KKKT Dayosisi ya kaskazini kati, kwa kumpa heshima kubwa ya kuwa mgeni rasmi katika uongozaji wa harambee ya ujenzi wa kanisa la KKKT Usharika wa Moivaro Arusha.
Kwa upande wake, askofu Laiser alisema mbali na washarika kuwa mstari wa mbele katika kumtolea mungu, aliwahimiza kujitokeza kwa wingi katika zoezi la sensa ya makazi na watu pamoja na kutoa maoni yao katika uundwaji wa katika mpya.
Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa jengo hilo la kuabudia lililopo mtaa wa Manemanet, mchungaji kiongozi wa KKKT Usharika wa Moivaro, Bw.Daniel Kambaine alisema hadi kufikia sasa jengo hilo limekwisha gharimu sh. milioni 133 ambapo wakristo wenyewe wamekwishachangia sh. milioni 84.
KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati Usharika wa Moivaro umeweka malengo ya kuhakikisha kuwa jengo hilo linamalizika na kuanza kutumika kabla ya mwanzo wa mwaka 2013.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment