17 August 2012

Wanaompinga Kadhi wajitoe katika Uislamu- Mufti Simba


Na Heri Shaaban

BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA ), limesema Waislamu wanaopinga uteuzi wa Kadhi Mkuu Shekhe Abdalah Yusuph, wanapaswa kujitoa katika dini hiyo.

Tamko hilo limetolewa Dar es Salaam juzi na Shekhe Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa bin Shaaban Simba katika futari ambayo iliandaliwa na Taasisi ya Kiislamu ya Imam Bukhary.


Shekhe Simba alisema uteuzi wa Kadhi wa Tanzania Bara umezingatia vigezo vyote vya dini hiyo hivyo Waislamu hawapaswi kumbeza wali wampe ushirikiano ili aweze kufanya kazi aliyopewa kwa faida ya Waislamu wote nchini.

“Utezi wake umezingatia vigezo vyote vya dini yetu, Waislamu wanaopinga uteuzi wake wajitoe na kujivua Uislamu,” alisema.

Aliongezea kuwa, baada ya uteuzi wa Kadhi, kundi la Waislamu lilianza kubeza uteuzi wake bila kujua mtu aliyepewa nafasi hiyo ni Mwanazuoni mzuri anayepaswa kupewa ushirikiano.

Alisema ombi la kudai Kadhi Mkuu limedumu zaidi ya miaka 27 akiwa na jukumu la kusikiliza ya Waislamu ambayo ni pamoja na migogoro ya ndoa, talaka na kusimamia mirathi.

Kwa upande wake, Shekhe Yusuph aliwataka Waislamu kumpa ushirikiano wa hali na mali ili aweze kutekeleza wajukumu aliyopewa kwa ufanisi mkubwa.

Aliongeza kuwa, hivi sasa ameanza kupokea kesi mbalimbali za waumini wa dini hiyo na kuzishughulikia zikiwemo za mirathi, talaka, ndoa na nyingine tayari amezitolea uamuzi.

Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Shekhe Khalifa Khamisi, aliipongeza BAKWATA kwa kufanikisha uteuzi wa Kadhi na Manaibu wake wawili Shekhe Abubakar Zuber na Ally Muhidini.

Akizungumzia sensa ya watu na maakazi, Shekhe Khamisi aliwataka Waislamu wote nchini kushiriki vyema, kuzingatia taratibu za kidini na kiibada ili kuunganika kiroho.

“Ni jambo la aibu sana kwa watu wazima wenye akili timamu tena Mashekhe wanaposimama kidete na kuwashawishi Waislamu kususia sensa ili kuikwamisha Serikali ishindwe kupanga mikakati mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi wake,” alisema.

No comments:

Post a Comment