10 August 2012

Wananchi washirikishwe kutunga sheria



Na Salim Nyomolelo

USHIRIKISHWAJI wa wananchi katika maamuzi na miradi ya maendeleo ni moja ya kigezo cha utawala bora.

Wananchi wakipewa nafasi ya kushiriki kutoa maoni yanayoweza  kubadili mfumo wa utendaji husaidia pia kupunguza ubadhirifu.


Serikali imekuwa ikifanya mambo mengi bila kuwashirikisha wananchi jambo ambalo linasababisha kutokea kwa migogoro katika jamii hasa baada ya jambo hilo kutokuwa na manufaa.

Licha ya wananchi, wanasiasa na wadau mbalimbali wa maendeleo nchini kupigia kelele kuhusu uboreshwaji wa katiba lakini hii iliyopo bado viongozi hawaifuati.

Kitendo cha viongozi wakuu wa serikali kufanya maamuzi yanayogusa maslahi ya wananchi moja kwa moja bila ya kuwashirikisha ni uvunjaji wa katiba ya nchi ambayo waliapa baada ya kuingia madarakani.

Ibara ya 8 ya katiba ya Tanzania inaeleza kuwa serikali itawajibika kwa wananchi na serikali itategemea ustawi wa wananchi ambapo inawataka viongozi pia kuwashirikisha wananchi katika mambo yanayogusa maslahi yao ambapo kufanya tofauti ni kuvunja katiba.

Kwa maana hii kuna mambo mengi yanayogusa maslahi ya watanzania ambayo viongozi wa serikali waliyafanya, wanafanya na wataendelea kuyafanya ambayo yanavunja katiba moja kwa moja.

Serikali kuchukua uamuzi wa kupitisha Sheria ya Mafao katika mabadiliko ya kupata mafao kwa wafanyakazi baada ya kustafu bila kupata maoni ya wafanyakazi ni kinyume cha katiba ya nchi ibara ya nane.

Viongozi wa serikali wamekuwa wavivu wa kufikiri kutokana na kushindwa kufanya utafiti wa kina kwa wafanyakazi ili kuweza kugundua aina za ajira walizonazo.

Watanzania wengi hawana ajira za kudumu na hivyo huingia katika ajira za mikataba ya kuanzia miezi mitatu na kuendelea ambapo ajira hizo zinakoma baada ya mikataba kuisha.

Ni ukweli usiopingika kuwa idadi kubwa ya watanzania wanafanyakazi katika kampuni binafsi ambazo hazina ajira za kudumu na wafanyakazi hutegemea mafao kuendesha maisha yao mara tu baada ya kumaliza ujira wao.

Kitendo cha serikali kusaini mabadiliko ya sheria hiyo bila kuangalia hali ya maisha ya mtanzania ni kinyume cha haki kwa maana ya ushirikishwaji katika maslahi yake na ni kinyume cha utawala bora.

Watanzania waliowengi ambao wanafanya kazi katika kampuni binafsi humaliza mikataba yao kabla ya miaka 55 ambapo kusubiria hadi kutimia kwa umri huo ni dhahiri kutawasababishia kuishi maisha ya shida.

Hivyo hivyo wapo ambao wanaofanya kwa mikataba ya kuanzia miezi mitatu hadi miaka kumi jambo ambalo halina tija kumsubirisha mstaafu hadi kufikia miaka 55 ndipo alipwe mafao yake.

Ikumbukwe kuwa mafao ya mstaafu ni haki yake ambapo inampasa kupata mafao hayo mara baada ya kustaafu ili kuweza kuinua maisha yake kwa kufanya miradi mbalimbali ya maendeleo.

Na kama hoja ya serikali kustaafu ni baada ya miaka 55 na ndipo mfanyakazi achukue mafao yake lakini kuna wazee ambao hufanya kazi mara baada ya kustaafu kwa njia za mikataba ambapo pia huifadhiwa mafao yao.

Lakini serikali imeshindwa kufafanua kuwa wale ambao wanaingia mikataba mara baada ya kustaafu watalipwa mafao yao wakiwa na umri gani?.

Idadi kubwa ya waliokuwa wafanyakazi wa jumuiya ya afrika ya mashariki waliingia katika mikataba mbalimbali ikiwamo katika kampuni za ulinzi ambao najiuliza wao watakuja kulipwa wakiwa na umri wa miaka mingapi kutokana na kupitishwa umri wa miaka 60 jambo ambalo hata serikali imeshindwa kulitolea maelezo wakati wa kuwasilisha sheria hiyo.

Serikali ilipaswa pia kufafanua utaratibu wa kulipwa mafao kwa wafanyakazi ambao huingia mikataba na waajiri wa kampuni mbalimbali baada ya kustaafu wakiwa na umri wa zaidi ya miaka 60.

Kwa hili nasema dhahili kuwa serikali imechemka na kama busara haitatumika linaweza kusababishia nchi kuingia katika machafuko yasiyo ya lazima, kwa sababu limegusa maslahi yao bila ya kushirikishwa.

Naiomba serikali kurudisha suala hili kwa wananchi pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo, ili lipatiwe mjadala mpana ambao utakuwa na baraka zote.

Serikali ni pamoja na wananchi na hivyo ikumbuke kuwashirikisha wananchi kwa mambo ambayo yanawahusu ama yanagusa maslahi yao na itekeleze ama kutotekelezwa kutokana na hoja zao.

Serikali lazima ithamini matakwa ya wananchi wake, utawala wa sheria pamoja na mambo yote ya msingi na kuondoa vikwazo visivyokuwa vya lazima.

Mungu Ibariki Tanzania
snyomo@yahoo.com
0715 654410

No comments:

Post a Comment