02 August 2012
Wana Tanga waishio Dar kukutana Agosti 15
Na Mwandishi Wetu
WAKAZI wa Dar es Salaam waliozaliwa mkoani Tanga, wanatarajia kukutana Agosti 15 mwaka huu, ili kujadili mambo mbalimbali yanayohusu Mkoa huo.
Miongoni mwa mambo ambayo yatajadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na kushuka kwa maendeleo ya sekta mbalimbali ikiwemo maji, elimu na kilimo cha mkonge hivyo kukwamisha maendeleo.
Akizungumza na Majira Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Wananchi wa Mkoa huo, Bw. Abdraham Lukindo, alisema mkutano huo utashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wasomi, wachumi, wafanyabiashara na viongozi wa Serikali.
Alisema wameamua kuitisha mkutano huo baada ya kuona Mkoa huo unakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zinachangia kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi.
“Hii ni fursa ya pekee kwa wazaliwa wa Mkoa wa Tanga wanaishi Dar es Salaam, kukutana pamoja na kujadili changamoto zilizopo ili kuchochea maendeleo ya kielimu, kiuchumi na kijamii.
“Mkutano huu utaibua mbinu na maarifa mapya ili kuuwezesha Mkoa wetu na watu wake kujikomboa katika lindi la umaskini,” alisema Bw. Lukindo na kuongeza kuwa, wanamini mkutano huo utahudhuriwa na wabunge wote wa Mkoa huo na Mawaziri.
“Imani yetu ni kwamba, kikao hiki kitakuwa na mafanikio makubwa kutokana na mawazo ambayo tutayapata kwa wenzetu, tunataka kuona bandari yetu ili ifanye kazi ipasavyo na kuingiza kipato cha uhakika kitakachoinua uchumi wa Mkoa na watu wake,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment