02 August 2012
Vigogo wa Jeshi kusomewa maelezo ya awali Agosti 30
Na Rehema Mohamed
UPANDE wa mashtaka katika kesi ya kula njama na matumizi mabaya ya madaraka inayomkabili Mkurugenzi wa Shirika la Uchumi la Jesji la Kujenga Taifa (SUMA JKT), Kanali Ayoub Mwakang’ata na maofisa wenzake, unatarajia kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa wa kesi hiyo Agosti 30 mwaka huu.
Hayo yalisemwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bi. Lizya Kiwia, mbele ya Hakimu Mkazi Aloyce Katema, wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.
Alidai kuwa, upelelezi wa kesi hiyo tayari umekamilika ambapo washtakiwa wengine ni Luteni kanali Mkohi Kichogo, Luteni Kanali Paul Mayavi, Meja Peter Lushika, Sajenti John lazier, Meja Yohana Nyichi na Mkurugenzi wa Miradi ya Matrekta wa shirika hilo, Luteni Kanali Felex Samillan.
Washtakiwa walifikishwa mahakama kwa mara ya kwanza Julai 2 mwaka huu, ambapo wanadaiwa kutenda kosa la matumizi mabaya ya madaraka kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007.
Ilidaiwa kuwa, Machi 5,2009 katika chumba cha mikutano cha ofisi ya SUMA JKT, Dar es salaam, wakiwa wajumbe wa Bodi ya Tenda ya shirika hilo, kwa makusudi walitumia madaraka yao vibaya.
Washtakiwa hao wanadaiwa kutoa maamuzi yalioonesha kutolewa na Bodi ya Wakurugenzi ya TAKOPA ili kununua magari na vifaa vya ujenzi bila kupata idhini ya bodi hiyo.
Machi 12,2012 washitakiwa hao wanadaiwa kupitisha maazimio ya kununuliwa magari na vifaa vya ujenzi vilivyotumika kinyume na kifungu cha 58( 3) cha Sheria ya Mamunuzi ya Umma mwaka 2005.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment