16 August 2012

Wakatwa mapanga, kuporwa mil. 1.7/-



Na Suleiman Abeid, Shinyanga

WATU watano wakazi wa Kitongoji Nyamhela, kilichopo kwenye Kijiji cha Mhongolo, Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, juzi walinusurika kufa baada ya kushambuliwa kwa kukatwa mapanga katika sehemu mbalimbali za miili yao na watu wasiojulikana.


Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Evarist Mangalla, alisema katika shambulio hilo watu hao walifanikiwa kupora sh. milioni milioni 1.7.

Alisema tukio hilo lilitokea saa saba usiku ambapo wanawake wawili wakazi wa kijiji hicho (majina yamehifadhiwa), mbali ya kujeruhiwa, pia walibakwa na watu hao.

“Watu waliojeruhiwa kwa kukatwa mapanga ni Bw. Nyerere Malimi (53) ambaye ndiye mmiliki wa nyumba iliyovamiwa, Bw. Marco William (18), Bw. Idebuke Manyanda (31), Bw. Mayira Pili (75) na Bw. Mateso Nyerere (26) wote wakazi wa kijiji hiki,” alisema.

Aliongeza kuwa, wanawake waliobakwa mmoja alikuwa na umri wa miaka 18 na mwingine 30 ambao wote walikimbizwa katika Hospitali ya Serikali wilayani humo ili kupatiwa matibabu.

Kamanda Mangalla alisema watu hao pia walipora simu mbili za mkononi aina ya Nokia na bego moja ambalo lilikuwa na nguo za aina mbalimbali.

Katika tukio lingine, mkazi wa Kijiji cha Nyihogo, wilayani hapa,  Bw. Paulo Joseph (19), naye amenusurika kufa baada ya kuvamiwa nyumbani kwake, kuchomwa kisu mgongoni na watu wasiojulikana.

Kamanda Mangalla alisema, tukio hilo lilitokea juzi saa saba usiku  ambapo hali ya Bw. Joseph ni mbaya na amelazwa katika Hospitali ya Serikali mjini hapa.

Alisema hadi sasa, hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na matukio hayo na kutoa wito kwa wananchi kutoa taarifa kituo chochote cha polisi wakimuona mtu au watu ambao wanawatilia shaka.


No comments:

Post a Comment