16 August 2012

'WAMA, EOTF hazitumii rasilimali za serikali'


Na Magreth Kinabo, Maelezo-Dodoma

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Utawala Bora, Kapteni mstaafu, George Mkuchika, amesema Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) na Taasisi ya Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF),  zilianzishwa na kuandikishwa kwa mujibu wa sheria inayotawala taasisi hizo na hazitumii rasilimali za Serikali.

Bw. Mkuchika aliyasema hayo bungeni mjini Dodoma jana wakati akijibu swali Mbunge wa Viti Maalum Bi. Naomi Kaihula (CHADEMA), ambalo liliulizwa na Mbunge wa chama hicho Viti Maalumu, Bi. Leticia Nyerere.

Katika swali lake, Bi. Kaihula alisema ipo tabia ya wake wa marais nchini kuunda taasisi 'NGO’S' na kuzisajili kama za kwao binafsi wakati zinatumia rasilimali za Serikali.

Je, ni lini Serikali itaweza utaratibu ambao utazifanya taasisi hizo ziwe za kisheria ili wake wa marais wanapomaliza muda wao wapokezane vijiti kana ilivyo katika naafasi ya urais.

Akijibu swali hilo, Bw. Mkuchika alisema ni kweli kuna taasisi ambazo zinaendeshwa na wake wa marais ambazo hufanya shughuli zake kama zilivyo taasisi nyingine zisizo za kiserikali.

Alisema ipo taasisi ya WAMA, ambayo imeanzishwa na Mama Salma Kikwete (Mke wa Rais wa Awamu ya Nne), na  EOTF  iliyoanzishwa na Mama Anna Mkapa (Mke wa Rais wa Awamu ya Tatu).

Aliongeza kuwa, kama zilivyo taasisi nyingine za hiari na zisizo za kiserikali (NGO,S), tasisi hizo ziliundwa kutokana na mke wa rais anavyopenda kujishughulisha na shughuli za kijamii.

“Inawezekana kabisa akatokea mke au mme wa rais ambaye hana utashi au mapenzi ya kujishughulisha na shughuli za kijamii ambapo kutokana na mazingira haya, Serikali haioni sababu za kuweka utaratibu wa kufanya taasisi hizi ziwe za kisheria,” alisema.

Alisema kwa kufanya hivyo, Serikali itakuwa inalazimisha wafanye shughuli wasizo na utashi nazo.

Akijibu swali la nyongeza la Bi. Nyerere, ambalo aliuliza Watanzania wananufaikaje na taasisi hizo bila tofauti za kiitikadi ambapo Bw. Mkuchika alijibu kuwa, hakuna anayefanya kazi kwa kubagua na kuzipongeza taasisi hizo kwa kufanya kazi mijini, vijijini na kuwataka wananchi kuanzisha taasisi kama hizo.

“Jumla ya wanafunzi  939 wamenufaika kielimu kupitia WAMA, ambayo pia imetoa msaada wa vitanda na magodoro katika wodi za wakina mama na sh. milioni mbili za ujenzi wa Hospitali ya wanawake ya MEWATA, ambazo ni msaada kutoka Taasisi ya Nakayama, iliyopo nchini Japan,” alisema.

Aliongeza kuwa, taasisi hiyo ina mpango wa kutoa vifaa vya hospitali vyenye thamani ya dola za Marekani milioni tatu kupitia msaada wa Project Care, Marekani ambapo taasisi ya EOTF imetoa mafunzo kwa wajasiliamali mbalimbali nchini.


No comments:

Post a Comment