09 August 2012

Wagombea CCM wajitenge na vitendo vya rushwa



CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kinaendesha maandalizi ya uchaguzi za ndani ili kuwapata viongozi wake kuanzia ngazi nchini katika  Jumuiya zake za Umoja wa Vijana(UVCCM) na ile ya Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT).

Miongoni mwa nafasi zinazowaniwa na wanachama wa chama hicho kupitia jumuiya hizo, ni  wenyeviti ,makamu wenyekiti na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa.

Tayari wanachama wengi wameonesha nia kuwania nafasi hizo kwa chukua na kurejesha fomu kwa mjibu wa taratibu, kanuni za sheria za uchaguzi zilizowekwa na chama hicho.

Hata hivyo,yapo  malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa kupitia vyombo vya habari nchini, kuwa wapo baadhi ya wagombea katika nafasi hizo, ambao wanatuhumiwa kutumia rushwa ili kushawishi wapiga kura kuwakubali.

Tunasema kuwa mgombea yoyote anayetoa rushwa katika uchaguzi si mwaminifu wala hana uzalendo  na chama chake. Tunasema hivyo kwa sababu wagombea wa aina hiyo hawana lengo kukifanya chama hicho kiendelee kusimamia misingi yake iliyowekwa na waasisi wake.

Wagombe wa nafasi hizo wa wapiga kura inabidi wakumbuke kuwa rushwa ni adui mkubwa wa maendeleo. Rushwa madhara makubwa na inachangia  kudumaza demokrasia badala ua kuishamirisha. Kwa msingi huo inafaa kupigwa vita na kila mpenda maendeleo kwa dhati.

Tunaamini hivyo,kutokana na ukweli ulio wazi kuwa mgombea yoyote anayetumia rushwa kuingia madarakani anakuwa  hana hoja za msingi za kukiendeleza chama, pili uwezo wake wa kuongoza ni wa kutilia shaka, kwani mgombea mahiri ni yule anayejiamini yeye binafsi kwa hoja na ana malengo ya kusaidia chama.

Tunachukue fursa hii, kuwaomba wagombea wote katika jumuiya hizo kuachana na tabia ya kutoa rushwa, kutokubali pia kutumiwa kwa lengo la kuwachafua wenzao ili wao waonekane bora zaidi na hatimaye waibuke na ushindi katika uchaguzi huo.

Tunatoa rai kwa wanachama ambao ni wapiga kura,nao waache kupokea rushwa, wakumbuke kwamba anayetoa na anayepokea wote nia yao ni moja, yaani kurudisha nyuma maendeleo pamoja na kuondoa misingi ya demokrasia ya utawala bora.

Katika kipindi hiki Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), iwe macho kuhakikisha rushwa haitumike kupata viongozi.

Tunaamini kuwa CCM ni chama kikongwe nchini hivyo katika uchaguzi huo kioneshe mfano kwa vyama vingine. CCM bila rushwa tunaamini inawezeka na huu ndiyo wakati mwafaka kwa chama hicho kudhihirisha hilo



1 comment:

  1. CCM NA RUSHWA NI DAMU DAMU. WALIKWISHA TANGAZA KUWA RUSHWA NA SAWA NA TAKRIMA. VIONGOZI MSIPOTEZE MUDA KUPIGA KELELE.

    ReplyDelete