22 August 2012
Viongozi waheshimu nyadhifa zao na jamii
Na Bryceson Mathias
KATIKA kile kinachoonekana kuwa, kauli nyingi za baadhi ya viongozi kukosa tafiti au zinatolewa kwa makusudi bila kujua kuwa wanapotosha mwelekeo wa Taifa hali hii imeota mizizi na kuzua mkanganyiko katika jamii husika.
Hata kama viongozi wetu wana utamaduni wa kurushiana vijembe baina yao au miongoni mwa vyama vya siasa, basi ni vema wakatambua kwamba, si kila kitu au mahali panatakiwa kutoa vijembe.
Nasema hivyo kwa sababu, kama mambo hayo yakitawala, ni ukweli usiopingika itaangamiza watoto waliopo na vizazi vinavyokuja tofauti na kuwa nyenzo ya maisha yao na jamii.
Mapungufu ya baadhi ya viongozi wetu ambao yu mkini saa nyingine wameparamia nyadhifa hizo kwa babati mbaya badala ya kuzaliwa nazo, sasa yamewafikisha hata kutoheshimu misiba na kuogopa vyombo vya dini kama ilivyokuwa enzi za mwalimu.
Kumekuwepo watu miongoni mwetu hawautendei haki umri na nyadhifa zao kwamba ni heshima.
Mara kadhaa viongozi nchini, wamekuwa wakilalamikia kuporomoka kwa maadili katika jamii na badala ya lawama hizo kuzielekeza kwa vizazi vya sasa na hasa watoto wetu, kumbe tunatakiwa kujielekeza vidole wenyewe kwa kushindwa kujiheshimu katika jumuiya zetu.
Kuna wakati wa kuomboleza na wakati wa kurukaruka, kukumbatia na wakati wa kuepuka kukumbatia pia, wakati wa kuacha kutafuta kilichopotea. Mtendaji ana faida gani katika jambo analofanyia kazi ngumu?
Katika hili nimekuja kujua kwamba hakuna jambo lingine bora kuliko mtu kufurahi na kufanya mema maishani mwake, lakini cha ajabu wapo watu wasioambilika, ambao wanaweza kupeleka kadi ya harusi na katika msiba.
Ni mara kadhaa kwenye misiba na sherehe mbalimbali tumeshuhudia vitu vya aibu na visivyo na ueledi wa kibinadamu, ambapo baadhi ya viongozi, wamekuwa wakitoa salamu zisizo na afya wala faraja ya maombolezo.
Ni hoja yangu kwamba, utamaduni wa namna hii kwa wanasiasa wanaotegemewa kuwa vioo vya na maadili mema halafu wanaiingiza jamii kwenye miiba ya utovu wa nidhamu, watafanya hayo mpaka lini?
Ndiyo maana wakati mwingine viongozi wa namna hii wakipita kwa wananchi ambao wamewaona wakizungumza mambo yasiyo ya msingi huzomewa, wananchi hawafanyi hivyo ili kuwakomoa hapana, ila kuna kitu kibaya wamewaona wakifanya na kuwashangaza.
Najiuliza, kwa nini viongozi tunaodhani huenda mna upeo wa hekima zaidi kuliko waliowachagua mnafanya hivyo? Kama ulichaguliwa na watu, au uliteuliwa, huoni kama kwa unayofanya unamdharirisha aliyekuchagua au kukuteua?
Tukikupa uongozi tunajua unaweza kutuongoza, haya yanayotokea yanatufundisha nini?
Ni vizuri Kiongozi ukipata nafasi za kuwafariji watu, fariji kiasi cha kuwafanya waliokata tamaa waone wamefarijiwa na kusahau ukiwa! Ukipata nafasi ya kuunganisha watu, unganisha waone hawatawaliwi na mkoloni.
Ni heri viongozi wasifanye vitu mpaka watu wanaanza kusema aheri atoke haraka kutokana na unavyowakera.
Wee Mungu, ni lini hasa, utamfinyanga mtu atakayezaliwa tena Tanzania, atakayekuwa kama Edward Moringe Sokoine?
Mungu usimfanye azaliwe nchi nyingine, maana tutamkosa, na akija kwetu atakuwa mkimbizi, ambaye atahitajika awe na kitambulisho cha Taifa, na hataruhusiwa kuwa kiongozi.
Aidha nakutaka Mungu umuumbe na akue haraka, aje afute machozi ya wajawazito wanaoteseka kwa kuzalia watoto chini ya miti, atakayepunguza bei za bidhaa na maisha magumu, atakayeondoa ufisadi uliokithiri na rushwa, atakayelinda madini na wanyama wetu waliporwa kwenda Ulaya, atakayerudisha viwanda na rasilimali zote mikononi mwa umma,
Tena Mtu huyo aweze kuondoa njaa, akomeshe mauaji na ajali za kila siku ambazo zimekosa dawa, atakayewakemea viongozi ambao ni ndumila kuwili na wenye visasi, atakayefufua matumaini ya wananchi wanaouawa nyamongo kama ndezi wa kitoweo kumbe ni watanzania ambao utu, rasilimali na haki yao imeuzwa.
nyeregete@yahoo.co.tz
0715-933308
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment