22 August 2012

Makarani wa Sensa watishia kutofanya kazi


Agnes Mwaijega na Salim Nyomolelo

MAKARANI walioshiriki semina kuhusu Sensa ya Watu na Makazi, wametishia kutofanya kazi hiyo kama Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), itashindwa kuwalipa posho zao za siku saba.

Wakizungumza na Majira Dar es Salaam jana, baadhi ya makarani katika Wilaya ya Kinondoni, Kata ya Makumbusho, walisema hawapo tayari kulipwa nusu ya fedha wanazodai.

Mmoja wa makarani hao (jina tunalo), alisema kwa mujibu wa dodoso za sensa, makarani wanatakiwa kulipwa posho zao kila wanapomaliza semina jioni.

"Kwetu imekuwa tofauti, hatujalipwa chochote hadi leo (jana), tumetumia fedha zetu kuja kwenye kituo cha mafunzo badala yake tunapewa pesa ya siku nne sh.sh.140,000 badala sh.245,000 kwa siku saba hivyo tumezikataa," alisema.

Karani mwingine Bw. Gandolf Mosha, alisema kama wahusika watashindwa kuwalipa kwa wakati, watafute makarani wengine wa kuifanya kazi hiyo kuanzia Agosti 26, mwaka huu.

Kati ya makarani hao 4,000, baadhi yao walidai kutokana na usumbufu wanaoupata, hata wakilipwa fedha zote hawapo tayari kuifanya kazi hiyo.

Wakati huo huo, baadhi ya makarani waliohitimu mafunzo hayo kwenye Kituo cha Tambaza, Dar es Salaam, nao wamelalamikia kitendo cha kutolipwa stahiki zao.

Wakizungumza kwa sharti la kutotaka majina yao yaandikwe gazetini, walisema licha ya kumaliza mafunzo hayo, Serikali imeshindwa kuwalipa posho zao ili wajiandae na kazi hiyo.

"Inasemekana makarani ambao watalipwa ni wale wa dodoso refu, sisi tunashukuru kupewa mafunzo na kuhitimu lakini inasikitisha hadi sasa kutolipwa posho zetu,"walisema.

Kwa upande wao, Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Manispaa ya Temeke, nao wamedai kukasirishwa na kitendo cha Serikali kutowashirikisha katika mchakato huo.

Akizungumza na Majira, Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Manispaa hiyo, Bw. Othmani Omari, alisema anatarajia kukutana na Mkuu wa Wilaya hiyo Bi. Sofia Mjema, ili kujadili suala hilo.

"Katika mchakato mzima wa Sensa ya Watu na Makazi, Wenyeviti hatukushirikishwa hivyo nitafanya mazungumzo na Mkuu wa Wilaya na kutoa ufafanuzi," alisema.

Baadhi ya Wenyeviti walisema, wameshindwa kutoa elimu kwa wananchi kwa sababu ya kutoshirikishwa katika hatua za maandalizi.

No comments:

Post a Comment