29 August 2012

Uongozi Yanga wamruka Saintfeit *Ujio wa Twite giza totoro


Na Zahoro Mlanzi

SIKU moja baada ya Kocha Mkuu wa timu ya Yanga, Tom Saintfeit kutangaza kuwepo na mechi mbili za kirafiki, timu hiyo imemruka kimanga kocha huyo kwa kusema mechi wanayoitambua ni dhidi ya Coastal Union itakayocheza Jumamosi kwenye Uwanja Taifa, Dar es Salaam.

Kocha huyo raia wa Ubelgiji alitamba leo kungechezwa mechi dhidi ya Mafunzo ya Zanzibar na Jumamosi wangeikaribisha, AFC Leopards ya Kenya katika muendelezo wa maandalizi ya Ligi Kuu Bara.

Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Louis Sendeu alisema wanashangaa kuwepo na taarifa hizo huku uongozi ambao ndiyo waratibu wakuu kutojua mechi hizo.

"Kiukweli hata sisi hizo taarifa tunazishangaa, lini kocha amezungumza hayo au watu mmemnukuu vibaya, kwani kawaida hutoa mapendekezo ya mechi anazotaka na kisha uongozi kuyafanyia kazi," alisema Sendeu.

Alisema mpaka sasa wao wanatambua kwamba wana mchezo Jumamosi dhidi ya Coastal Union ya Tanga na kwamba timu hiyo, inaendelea na mazoezi kama kawaida kwa ajili ya mechi hiyo.

Sendeu alisema itabidi wazungumze naye kujua kitu gani ambacho kimetokea mpaka akazungumza hayo, inawezekana akawa na mipango ya kucheza na timu hizo, lakini uongozi ukawa hauna taarifa rasmi.

Wakati huoho, Katibu Mkuu wa timu hiyo, Celestine Mwesiga alipoulizwa kuhusu ujio wa beki mpya, Mbuyu Twite kutoka Rwanda, alisema: "Hatoweza kufika leo (jana) kama ilivyotarajiwa ila naomba unipigie simu baada ya nusu saa nitakuwa na uhakika lini atakuja.

Gazeti hili lililompigia baada ya dakika 30 alijibu: "We jua hafiki leo na mpaka sasa sijapata taarifa zozote ni siku gani atatua nchini.

Beki huyo ambaye amejizolea umaarufu kwa nyakati tofauti akiwa na timu ya APR ya nchini humo, alisajiliwa na Yanga hivi karibuni lakini usajili wake ulionekana kuwa na utata baada ya mahasimu wao wa jadi, Simba kudai walimsajili kabla.

Kutokana na utata huo, Simba ilitaka irudishiwe fedha zao ambazo mchezaji huyo ilidaiwa kuzichukua ikiwa ni sehemu ya makubaliano yao ya usajili, ambapo pia walitishia akitua nchini watamkamata na kumfikisha katika vyombo vya sheria.

No comments:

Post a Comment