29 August 2012

Filamu ya Yondan, Redondo kumalizika Jumapili



Na Zahoro Mlanzi

SAKATA la wachezaji Kelvin Yondan wa Yanga na Ramadhan Chombo 'Redondo' wa Simba, linatarajiwa kufikia tamati Jumapili baada ya Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji chini ya Mwenyekiti wake, Alex Mgongolwa kukutana kupitia usajili wa wachezaji kwa msimu wa 2012/2013.


Wachezaji hao kwa nyakati tofauti walijikuta katika wakati mgumu, baada ya kuhama toka timu moja kwenda nyingine huku kukidaiwa kuwa bado na mikataba na timu wanazotoka na mwingine kudaiwa makubaliano hayakufikiwa.

Yondan alisajiliwa Yanga, akitokea Simba huku ikidaiwa bado ni mchezaji wao halali kwa kuwa ana mkataba na Redondo, naye aliyesajiliwa akitokea Azam FC ikidaiwa bado ana mkataba wa mwaka mmoja.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpiwa wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema kamati hiyo itakutana kupitia masuala yote ya usajili pamoja na pingamizi zilizowekwa kwa baadhi ya wachezaji.

"Usajili utakaopitiwa ni kwa wachezaji wa Ligi Kuu Bara na wale wa Daraja la Kwanza kwa ajili ya msimu ujao na kuweka sawa baadhi ya mambo hususani kuna baadhi ya wachezaji wamewekewa pingamizi au kuonekana kusajiliwa katika timu mbili," alisema Wambura. 

Usajili utakaopitiwa ni wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL), ambapo Kamati itapitia pingamizi zilizowasilishwa na klabu mbalimbali dhidi ya wachezaji waliosajiliwa na klabu zingine.

Alisema kwa wale ambao bado wanazitumikia klabu zao kwa maana wana mikataba inayoendelea hawataguswa na suala hilo na kwa wale waliowekewa pingamizi, kama kutahitajika ushahidi italazimika klabu husika kuwa na vielelezo vitakavyothibitisha uhalali wa mchezaji husika.

Katika hatua nyingine, Wambura alisema Klabu ya Simba, imewasilisha vielelezo TFF juu ya uthibitisho wa usajili wa wachezaji Pascal Ochieng na Salum Kinje, ambapo sasa TFF inalishughulikia suala hilo kwa kuingiza vielezo hivyo kwenye Mfumo wa Uhamisho wa Wachezaji (TMS).

No comments:

Post a Comment