07 August 2012

Umaskini uliokithiri unatishia amani katika Taifa



Na Alfred Mwahalende

TANZANIA ni miongoni mwa nchi duniani inayosifiwa kuwa na amani ya kudumu tangu kupata uhuru.

Ni miongoni mwa mataifa yasiyo na historia ya vita duniani na kupata uhuru wake bila kumwaga damu.

Aidha mataifa ya kigeni yanapenda kuja kuwekeza  miradi na makazi huku wanaosikia habari zake wakitamani kufika
kuiona amani inayosikika kote ulimwenguni.

Ni dhahiri kwamba Tanzania imebarikiwa kuwa na hali ya hewa nzuri, mbuga za wanyama, rasilimali za kutosha, maliasili ardhi na madini, misitu, milima na mabonde ambayo pekee yanaifanya kuonekana katika mitazamo tofauti tofauti na hivyo kuwafanya watu wengi kuja kutalii na kufanya makazi au uwekezaji.

Kwa tafakari ya kawaida hapa utagundua amani tunayoisema  ni ile ya kutokuwa na vita, mizozo, malumbano, migogoro miongoni mwao.

Aidha katika nchi yenye vita huwezi kufanya kitu chochote badala yake watu wa taifa husika watakuwa ni wakimbizi na wageni wataogopa kuja kuwekeza katika nchi hiyo.

Mwanzoni mwa miaka ya 1945 baada ya vita vya pili ya dunia, Afrika kuliibuka vuguvugu la kudai uhuru miongoni mwa nchi wataliwa.

Wakati huo nchi nyingi za Afrika zilikuwa zinatawaliwa na mataifa ya nchi za magharibi kama Ujerumani, Uingereza,  ufaransa, Ureno na Ugiriki.

Aidha katika kudai uhuru wake nchi hizo zilitumia njia tatu, ambazo moja ni njia ya kudai uhuru kwa kumwaga damu au njia ya mtutu wa bunduki, pili kudai uhuru kwa njia ya kufanya mapinduzi na tatu njia ya amani.

Historia inaonyesha kwamba katika kujipatia uhuru wake nchi nyingi za Afrika zilipata uhuru  kwa njia ya vita na umwagaji damu.

Njia hii pekee inazijengea sifa mbaya ya kuwa nchi za vurugu na zisizotaka makubaliano katika kufanya  mambo  na mipango yake.

Tanzania ilitumia njia ya amani ambayo pekee inaijengea sifa kubwa miongoni mwa mataifa ya Afrika na duniani kwa ujumla.

Na hii itakumbukwa kwamba hata mara baada ya kupata uhuru bado Tanzania iliendelea kuwaheshimu nchi watawala bila kulipiza kisasi kama ilivyokuwa kwa wengine.

Katika historia ya amani iliyopo usipo mkumbuka baba wa taifa
mwalimu Julius Nyerere kwa jitihada zake kke katika kulipigania taifa kupata uhuru wake pasipo vita pia, kuliongoza taifa kwa amani ya kudumu.

Katika uhai wake mwalimu alipigania sana suala la
amani ambalo kwa kiasi kibwa linapigiwa kelele na mataifa mengi dunia na mwasisi wa usuluhishi wa migogoro katika nchi za Afrika na mataifa mengine duniani.

Kama utakuwa unashuhudia kinachoendelea katika nchi kama
Somalia, Tunisia, Syria, Misri na Libya umbuka kilio cha baba wa taifa kuhusu amani barani  Afrika.

Katika matazamo huu wa kuingalia tanzania kama nchi  ya amani watu wanatumia vigezo vya utulivu na upendo nchini.

Katika utamaduni wa watu ambao sitausahau ni amani ya watanzania, tena wale wanaoishi katika maisha ya kawaida na wageni wanaingia kila iitwapo kesho.

Lakini kama tutaendelea kusifia amani hii pasipo kurejea misingi ya haki na usawa miongoni mwa Watanzania itakuwa ni sawa na kazi bure. Amani ni usalama katika haki na usawa miongoni mwa jamii na hudhihirika katika utekelezaji na utoshelevu wa mipango bila ubuguzi utulivu wa watu wengine.

Katika maana hii utaweza kujiuliza maswali, je mauji ya albino nchini ndiyo amani tunayojivunia? ukatili dhidi ya watoto yatima na walemavu ndiyo amani tunaisema? ukatilii juu ya wafanyakazi katika sekta mbalimbali ndiyo misingi ya Tanzania? kutokuhoji mambo na kuonyesha hisia ndiyo chanzo cha amani tunayosifiwa na mataifa mengine?

Kutokana na kwamba miongoni mwa watanzania bado kuna watu wanaendelea kuangamia kutokana na vurugu na matukio yanayoendelea utakuwa ni shahidi kwa matukio ya ukatili yanayoendelea nchini.

Mambo kama haya tumezoea kuyasikia kwenye nchi za kidikteta na kuongozwa kiimla ambapo watawala badala ya kutumia njia ya kidemokrasia na kisheria kushughulikia wanaoamini ni maadui zao katika utawala, hutumia wahuni kuwatesa, kuwafunga na hata kuwaua.

Sitaki kuamini kwamba Tanzania imefikia huko ukatili huo pekee unaashiria watu wenye mioyo migumu kiasi cha kushindwa
kuwa hata angalau na utu na uvumilivu.

Pia katika suala la maandamano yanayofanywa nchini na vikundi
mbalimbali vya wanaharakati vinaashiria moja kwa moja kukosekana kwa amani ambayo bado tunaendelea kujivunia pasipo kuangalia haki na usawa kama vinatiliwa mkazo.

Tanzania ni jambo la kawaida kufanya utekelezaji wa sera na mipango mpaka pale watu wanapoandamana, kitendo hiki  kinachochea hali ya kukosekana kwa amani miongoni mwa wananchi hata kama kuna watu wanatusifia.

Aidha  kitendo cha askari kutumia mabomu kuwatuliza  na kuwatawanya watu wakati kufanya maandamano  kudai haki zao za msingi kinaashiria kukosekana  kwa amani miongoni mwa wazawa na inabaki katika historia na nadharaia na badala yake hatuwezi kufikia kilele cha amani ya kudumu.

Kama utaratibu huu  utaendelea kutumiwa na watawala kama njia pekee ya kutatua matatizo na itakuwa ni njia ya kuwapa kiburi watanzania kiasi kwamba baadaye nchi inaweza kuingia katika machafuko yasiyovumilika kiasi kwamba jeshi linalotumika kutuliza amani litashindwa kufanya kazi na ndiyo mwazo wa vita miongoni mwetu.

Kadhalika utakumbuka tofauti iliyopo kati ya walionacho na wasionacho (maskini na tajiri). Katika nchi ya Tanzania utabaini kuwa kuna utofauti mkubwa hali inayobainisha moja
kwa moja kukosekana kwa usawa miongoni mwa wananchi.

Kitendo hiki kinawanyima amani watu wa hali ya chini kwani hawawezi kuyafurahia maisha yao.

Hata hivyo utofauti unafanywa na viongozi wa ngazi za juu katika serikali unawapa hasira wananchi kutokana na kwamba hakuna hatua zozote za kisheria zinazochukuliwa dhidi ya  vitendo hivyo.

Katika mtazamo wa kawaida wapo watanzania wanaojilimbikizia mali huku wakiendelea kuwakandamiza wengine na ambao kwa bahati mbaya ndiyo wavuja jasho, asilimia  kubwa ya wakulima wanafanya kazi usiku na mchana lakini bado hali zao ziko matatani na wakati mwingine wanakosa hata mlo mmoja  kwa siku.

Hebu tujiulize amani tunayojivunia ni hii ya kutofautiana kimaendeleo miongoni mwetu kiasi kwamba hatukuzaliwa na kukulia katika nchi moja ambayo kila siku inasemwa maskini.

Je, umaskini tunaousema ni ule wa kukosa  kunufaika na maliasili zetu na badala yake kuwanufaisha wachache? kama jibu ni ndiyo kwa nini tuendelee kulea mifumo inayowanufaisha wachache na badala yake wengi kukosa amani ya kuwa wazawa katika nchi yao?

Kama utataka kusoma hali ya hewa ya taifa letu kumbuka mara baada ya kukamatwa mwizi wa kuku, jinsi anavyoshughulikiwa, wakati mwingine kumchoma moto. Katika mtazamo wa kibinadamu hapa inaashiria ukosefu wa mioyo yenye upendo miongoni mwetu.

Kadhalika kama amani tunayojivunia itakuwa ni ile ya
utulivu, kukosekana kwa vita, upendo, makubaliano hatuna budi kurudia utamaduni wetu wa usawa na haki miongoni mwetu pasipo ubaguzi ya rangi wala dini. Kwani umaskini ndio utachangia kuvuruga amani iliyopo.

Mwandishi ni mwanafunzi wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam 0758051641 mwahalendealfred@yahoo.com

1 comment: