07 August 2012

Serikali kujenga uwanja kwa ajili ya wakulima


Na Allan Ntana, Tabora

MKOA wa Tabora umeazimia kujenga uwanja mpya wa kisasa utakaoanza
kutumika mwakani katika Maonesho ya Siku ya Wakulima ‘Nane Nane' ambayo kilele chake hufanyika Agosti 8, kila mwaka nchini.

Akihutubia wananchi katika uzinduzi wa maonesho hayo, Mkuu wa mkoa huo Bi. Fatma Mwassa mwishoni mwa wiki katika Uwanja wa Ipuli alisema uwanja huo sasa wanataka ujengwe ili uwe wa kisasa zaidi.

Bi. Mwassa aliongeza kuwa katika maonesho yajayo mwakani uwanja huo utakuwa umefanyiwa mapinduzi makubwa na utakuwa wa kisasa na kazi inaanza mara baada ya maonesho ya maka huu kufikia tamati.

Alisema kuwa, mwakani wataalika wakulima na wadau mbalimbali wa kilimo kutoka mikoa yote ya kanda hususan mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora yenyewe ili kujionea shughuli mbalimbali za uzalishaji katika mabanda ya wakulima.

Aidha Bi. Mwassa aliitaka kila halmashauri kuwahamasisha wakulima
kuongeza uzalishaji kuanzia vijijini hadi mijini ikiwa ni pamoja na
kuwakopesha vijana fedha za kutosha uzalishaji ili washiriki
kikamilifu katika maonesho ya mwakani.

Pia alisisitiza juu ya umuhimu wa kulima mazao ya bustani kama vile mboga mboga, vitunguu, matunda na mtama mweupe kwani mazao hayo yanaweza kumwinua mkulima wa kipato cha kawaida kwa muda mfupi kwa kuwa yanauzika zaidi.

Hata hivyo Mratibu wa Sherehe za Maonesho hayo mkoani Tabora Bw. Daniel Moshy
ambaye ni Ofisa Kilimo wa Manispaa ya Tabora alisema, lengo la
maonesho hayo kwa mwaka huu ni kuonesha mbinu mbalimbali za namna
ya kuendesha kilimo cha kisasa.
*****

LEAD

Barwany aishukia Serikali,
imeipuuza mikoa ya Kusini

Na Mwandishi wetu, Dodoma

MBUNGE wa Lindi Mjini Bw. Salum Khalfan Barwany ameishukia Serikali na kudai kuwa inachangia kwa kiasi kikubwa kuwasababishia umaskini wananchi wa mikoa ya Kusini.

Hayo aliyasema mwishoni mwa wiki Bungeni mjini Dodoma, alidai Serikali kwa makusudi inachochea umaskini baada ya kushindwa kuviendeleza viwanja vya ndege.

Bw. Barwany alisema kuwa inasikitisha kuona serikali inavyotelekeza viwanja vya ndege pamoja na bandari bila kutambua kuwa kwa kufanya hivyo ni kuendelea kuwachimbia shimo la umaskini.

Alisema kuwa, inasikitisha kuona kuwa kila mara mikoa ya Lindi na Mtwara imekuwa haipangiwi fedha za maendeleo wakati mikoa mingine imekuwa ikitolewa fedha za maendeleo.

Alisema, Serikali pamoja na kutambua kuwa mikoa hiyo ina rasilimali nyingi kama vile uchimbaji wa madini ikiwemo gesi bado kunaonekana kuwepo kwa upendeleo wa wazi katika mikoa mingine.

Mbali na hilo Bw. Barwany alisema kuwa serikali ya CCM imewageuza wananchi wa mikoa hiyo kuwa mtaji wao wa kisiasa kwa kuwaacha kuwa maskini ili wapate muda wa kuwarubuni kwa ahadi za kimaendeleo.

“Wana-CCM wamekuwa wakitumia umaskini wa wananchi hao kwa kuwaelezea kuwa watawapatia maendeleo ya kujenga bandari na viwanja vya ndege, kutokana na ahadi hizo wananchi wamekuwa wakiwaamini na kuwapigia kura lakini ahadi hizo hazitekelezeki,”alisema
************
3TH

Nyamwaga Tarime
hawana choo

Na Timothy Itembe, Mara


MJI wa Nyamwaga kata ya Nyamwaga Wilaya ya Tarime mkoani Mara ambao ni Makao Makuu ya Tarafa ya Ingwe hauna choo hali ambayo ni hatari kwa afya ya wakazi wanaozunguka mji huo pamoja na vitongoji vyake.

Licha ya kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime inakusanya mapato ya ushuru wa mnada na kwa wafanyabiashara wadogo sanjari na makato ya kodi mbalimbali zinazotokana na fidia kutoka migodi ya madini ya dhaabu, mji huo umekosa huduma hiyo muhimu.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bw. Lukas Ngotto wilayani humo, mwishoni mwa wiki alikemea kitendo hicho na kudai kuwa ipo haja Halmashauri ya Tarime kuboresha mazingira ya mji kuliko kujali
kukusanya mapato toka kwa wananchi huku wananchi wake wakiishi na kufanyia
biashara mazingira ambayo ni hatari kwa afya zao.

Kauli hiyo aliitoa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika mwishoni mwa wiki katika viwanja vya Ofisi ya CHADEMA Kata ya Nyamwaga wakati akihutubia wananchi mbalimbali.

"Mji huu ni mkubwa na huenda kama Wilaya ya Tarime ikigawanywa na kuwa na majimbo mawili ya uchaguzi utapendekezwa kuwa makao makuu ya jimbo, pia halmashauri inakusanya ushuru kutoka kwa wafanyabiashara wa soko la mnada wa ngo'mbe, mbuzi na bidhaa mbalimbali.

K"ama vile mitumba ya nguo kila siku za Alhamisi pamoja na kodi zingine zinazotozwa na kijiji kama vile asilimia kadhaa ya fedha ya watu wanaolipwa
fidia na mgodi, ambazo hubaki kijijini hapo kwa ajili ya maendeleo lakini bado mji hautamaniki, mazingira yake ni machafu na hauna choo," alisema Bw. Ngotto.

No comments:

Post a Comment