07 August 2012
TPBC yabariki SHIWATA kuandaa mashindano
Na Peter Mwenda
MTANDAO wa Wasanii Tanzania (SHIWATA), imepata kibali cha kuandaa mashindano ya ndondi za kulipwa kutoka kwa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC) kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Julai 24, mwaka huu.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Viwango vya TPBC, Boniface Wambura alisema kibali hicho kinaruhusu SHIWATA kuandaa mapambano na kwa kuanzia itaandaa kati ya Alfonce Joseph (Mchumiatumbo) na David Mlope (Zola D) litakalofanyika katika Tamasha la Watani wa jadi katika Sikukuu ya Idd El Fitri kwenye Uwanja wa Chuo cha Bandari, Temeke.
Alisema pambano hilo limeandaliwa na SHIWATA ili kukusanya fedha za ujenzi wa nyumba za kisasa za gharama nafuu kwa ajili ya wasanii, waandishi wa habari na wanamichezo katika Kijiji cha Mwanzega, Mkuranga.
Alisema pambano hilo litakuwa katika uzani wa juu raundi nane na pia kutakuwa na pambano moja la utangulizi.
Naye Mwenyekiti wa SHIWATA, Cassim Taalib alisema pamoja na pambano hilo, kutakuwa na mechi ya mpira wa miguu kati ya Simba na Yanga (Maveteran) katika Uwanja huo huo na mshindi wa mechi hiyo atazawadiwa ng’ombe dume.
Taalib alisema siku hiyo kutakuwa na burudani mbalimbali kutoka kwa Kikundi cha Mchiriku cha Jagwa, Roman Mg’ande wa Msondo atapigana mieleka na Lumole Matovolwa, Sophia Lubuva wa Simba atapambana na Mwajuma Jimama wa Yanga huku washangiliaji wa Mpira Pesa (Simba) watapambana katika mpira wa miguu na Watani wao wa jadi, Yanga Bomba.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment