Na Zahoro Mlanzi
WAKATI dirisha la usajili kwa wachezaji wa Ligi Kuu Bara likitarajiwa kufungwa leo saa sita usiku, wachezaji wa Yanga Jeryson Tegete na Shamte Ally, wameonekana kuiumiza kichwa Kamati ya Usajili ya timu hiyo baada ya kufanya kikao kila kukicha bila majibu.
Wachezaji hao inadaiwa watatolewa kwa mkopo kwenda kuchezea Toto African ya Mwanza, baada ya viwango vyao kuonekana vimeshuka lakini kumekuwa na mvutano miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo kuhusu uamuzi huo.
Akizungumza makao makuu ya klabu hiyo Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu alisema bado haijatangazwa rasmi kuwapeleka kwa mkopo wachezaji hao au wengine, ila kamati husika tangu juzi inafanya vikao vingi kujadili suala hilo.
"Kuhusu suala la kuwatoa wachezaji kwa mkopo, bado halijaamuliwa ila kamati tangu jana (juzi) na leo (jana) inaendelea na vikao kujadili usajili kwa ujumla na kama itaonekana kuna umuhimu wa kufanya hivyo itawekwa wazi," alisema Sendeu.
Mbali na hilo, pia alizungumzia kuhusu timu yao kupiga kambi nje ya nchi, ambapo alisema mpango huo upo ila wanaendelea kukamilisha baadhi ya vitu katika safari hiyo.
Alisema kama mambo yatakwenda vizuri walipanga kwenda nchini Rwanda, lakini mabadiliko yatakapotokea watajua waende nchi ipi na watakaa huko kwa wiki moja.
Aliongeza kuwa kikosi chao kwa sasa kimekamilika baada ya wachezaji, Juma Abdul na Salum Telela ambao walikuwa majeruhi kuanza mazoezi na wenzao na wapo vizuri sasa kwa ajili ya mashindano.
Pia alizungumzia ujio wa beki mpya kutoka APR ya Rwanda, Mbuyu Twite ambapo alisema atatua nchini wiki hii na wanatarajia atapata mapokezi makubwa kutoka kwa mashabiki na wanachama wao.
Alisema kwa sasa yupo kwa wazazi wake jijini Kinshasa, baada ya kutoka Lubumbashi ambapo amekwenda kupata baraka za wazazi wake ndipo aje kuitumikia timu hiyo.
No comments:
Post a Comment