16 August 2012
Dkt. Ulimboka ajipanga kulipuka *Madaktari sasa waibembeleza serikali
Na Waandishi Wetu
SIKU moja baada ya kuwasili kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dkt. Steven Ulimboka akitokea nchini Afrika Kusini ambako alikuwa akipatiwa matibabu, Watanzania wenye shauku ya kutaka kujua kilichomsibu wametakiwa kuwa na subira.
Baadhi ya madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), waliyasema hayo Dar es Salaam jana baada ya kuzungumza na Majira ili kujua mazingira ya kutekwa kwake.
“Kwanza tunamshukuru Mungu kutokana na afya ya mwenzetu kuimarika, wakati ukifika kila kitu kitawekwa hadharani kupitia vyombo vya habari, Dkt. Ulimboka atawaeleza Watanzania tukio zima la kutekwa kwake lilivyokuwa.
“Tunafahamu kila mtu ana shauku ya kumsikia akizungumzia tukio zima hadi kutupwa Msitu wa Mabwepande,” walisema.
Walisema licha ya kuwepo vitisho kwa baadhi ya viongozi wa jumuiya hiyo, wanaiomba Serikali kukutana na viongozi wao ili kumaliza mgogoro uliopo kati yao.
“Serikali ione umuhimu wa kusikiliza madai yetu, isisubiri kupelekewa taarifa ambazo wakati mwingine zinapotoshwa na kusababisha malumbano yasiyo na tija.
“Tunafahamu kuna kesi za viongozi wetu Mahakamani lakini ni vyema Serikali ikamaliza tatizo lililopo kwa kukaa mezani na viongozi wetu,” alisema daktari mmoja ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
Alisema kurejea kwa Dkt. Ulimboka akiwa mzima kumeongeza ari ya madaktari kufanya kazi kwani awali ilikuwa vigumu kuamini kama mwenzao afya yake imeimarika.
“Tulikuwa tukipata taarifa kuwa mwenzetu anaendelea vizuri lakini ilikuwa vigumu kuamini tofauti na sasa kwani tumemuona kwa macho yetu na kuzungumza naye,” alisema.
Hata hivyo, Katibu wa jumuiya hiyo, Dkt. Edwin Chitage, alisema madai ya madaktari si kuongezea mshahara tu bali ni pamoja na kuboreshwa kwa mazingira ya kazi.
Alisema madaktari wana malalamiko mengi ambayo yanapaswa kupatiwa ufumbuzi ili waweze kufanya kazi katika mazingira ambayo si hatarishi.
“Mazingira ya kazi yanatufanya tusiwe na ari ya kujituma kikamilifu, huwezi kumtibu mgojwa akiwa amelala sakafuni sambamba na ukosefu wa baadhi vifaa,” alisema Dkt. Chitage.
Akizungumza na Majira kwa njia ya simu kutoka jijini Mwanza, Katibu wa Chama cha Madaktari nchini (MAT), Dkt. Rodrick Kibangilia, alisema hivi sasa wanafanya utaratibu za kuzungumzia tukio hilo kupitia vyombo vya habari.
“Kwa sasa naomba tumwache apumzike, kuna maandalizi ambayo yanafanyika ili tuweze kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu mazingira ya kutekwa kwake,” alisema.
Taarifa ambazo gazeti hili limezipata kutoka MNH, zinasema jana madaktari walikuwa na kikao kizito lakini haikufahamika mara moja walikuwa wakijadili mambo gani.
Imeandaliwa na Rehema Maigala, Grace Ndossa, Stella Aron na Neema Malley.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment