16 August 2012
Stars uwanjani leo Botswana
Na Zahoro Mlanzi
TIMU ya Taifa ya soka 'Kilimanjaro Taifa Stars', leo itajitupa uwanjani kuumana na Botswana katika mechi ya kirafiki ya kimataifa itakayopigwa usiku kwenye uwanja wenye nyasi bandia nje kidogo ya jiji la Gaborone.
Stars iliondoka alfajiri ya jana ikiwa na kikosi cha wachezaji 17 huku ikiwakosa nyota wake Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengi waliozuiwa na timu yao ya TP Mazembe, kipa Deogratius Munishi na Shomari Kapombe ambao ni majeruhi.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Angetile Osiah alisema mara ya mwisho kuwasiliana na timu hiyo ilikuwa saa mbili asubuhi baada ya kufika jijini Nairobi na kwamba ana imani walifika salama Gaborone.
"Nilizungumza nao wakiwa Nairobi na mpaka muda huu (jana mchana), sijapigiwa simu inaonekana hakuna baya lililotokea ambapo wakitua Gaborone, watapumzika kidogo kabla ya kwenye kwenye mji ambao watachezea mechi hiyo," alisema Osiah.
Alisema kutoka Gaborone mpaka katika mji huo ni mwendo wa saa mbili, ambapo kwa mujibu wa ratiba ya mechi hiyo itachezwa usiku katika uwanja wenye nyasi bandia.
Katibu huyo alisema kikosi hicho kimeongezwa nguvu na wachezaji Simon Msuva, Omega Seme na Ramadhan Singano ambao walikuwa katika timu ya vijana (U-20), ambao walijiunga juzi usiku.
Akifafanua kuhusu kuchezwa usiku, alisema kwa mujibu wa Kocha Kim Poulsen, alipendekeza kwanza ni lazima ipatikane mechi ya kirafiki ili vijana wake wapate uzoefu na hata ilipopangwa usiku alisema ni jambo zuri.
Alisema timu hiyo itakapomaliza mechi hiyo itarejea nchini na wachezaji wataruhusiwa kurudi katika klabu zao kuendelea na majukumu mengine.
Katika hatua nyingine, Osiah akizungumzia usajili ambao inafungwa leo alisema mambo yote yaliyojitokeza katika kipindi hiki yatafanyiwa kazi na Kamati ya Sheria, Maadili, Hadhi kwa wachezaji ya shirikisho hilo ambayo itakutana hivi karibuni.
Alisema mpaka kufikia Agosti 10, mwaka huu ni timu za Azam na Kagera Sugar, ndizo zilizowasilisha usajili wao ambapo kesho wataanika majina ya wachezaji kwa timu zote.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment