22 August 2012

Tanga amwekea ngumu Aden Rage


Na Zahoro Mlanzi

RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amekataa barua ya kuomba kujiuzulu ya Mjumbe wa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF, Aden Rage.


Rage ambaye pia ni Mwenyekiti wa Simba alimuandikia, Tenga barua ya kujiuzulu wadhifa huo kwa kile alichosema 'kamati hiyo kushindwa kwa makusudi kusimamia sheria na kanuni za uendeshaji wa mpira Tanzania zinavyoeleza.'

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura alisema Tenga amekataa ombi hilo kutokana na maelezo ya Rage kuwa kama amehisi kuwepo udhaifu wa kutosimamia sheria na kanuni kama inavyotakiwa, ni vyema akaendelea kuwemo kwenye kamati hiyo ili kutoa msaada zaidi.

"Kutokana na uzoefu na uwezo ambao, Rage anao katika uongozi wa mpira wa miguu ni vyema akautumia kuisaidia kamati kutekeleza wajibu wake, kama inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria ili kusaidia kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya mpira wa miguu," alisema Tenga.

Alisema ni muhimu kwa mpira wa miguu kuongozwa kwa kufuata sheria na kanuni zilizopo na si katika kamati hiyo, ila kwa kamati zote za shirikisho hilo ili kuhakikisha mpira wa miguu unaongozwa bila kuonea wala kupendelea upande wowote.

Wambura alisema imesisitizwa kuwa kamati hazina budi kuchukua hatua zinazostahili bila woga pale kanuni zinapotaka hatua kuchukuliwa.

"Kamati zisisite kwa namna yoyote ile kuchukua hatua kwa vile kwa kufanya hivyo, uwezekano wa kutokea upendeleo au uonevu utapungua, hivyo mpira wa miguu kuongozwa kwa sheria na haki.

Wakati huohuo, TFF imeandaa semina kwa ajili ya makamishna, watathmini wa waamuzi na waamuzi wa Daraja la Kwanza, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Ligi Kuu inayotarajia kuanza baadaye mwezi ujao.

Kwa mujibu wa Wambura, makamishna na watathmini wa waamuzi, semina itafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Agosti 29-30 mwaka huu. Washiriki wanatakiwa kujigharamia kwa kila kitu; usafiri, malazi na chakula wawapo kwenye semina.

No comments:

Post a Comment