27 August 2012

Simba yazuru TBL Arusha


Na Mwandishi Wetu, Arusha

TIMU ya Simba ambayo imeweka kambi mkoani Arusha,   imefanya ziara ya kutembelea Kiwanda cha kutengeneza Bia Tanzania (TBL) kilichopo jijini hapa.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi wa timu hiyo, Ibrahimu Masoud 'Maestro' alisema wameamua kufanya ziara katika kiwanda hicho na kujionea mambo mbalimbali yanayofanywa na kampuni hiyo inayozalisha bia ya Kilimanjaro Lager ambayo ndio wadhamini wakuu wa timu yao.

Alisema kampuni hiyo imekuwa ikiwapa ushirikiano mkubwa katika mambo mbalimbali ya kimichezo ikiwa ni pamoja na kuwapatia magari ya usafiri, jezi pamoja na vifaa mbalimbali vya michezo, hivyo wamefurahishwa sana na jinsi walivyopokelewa vizuri kiwandani hapo na aliwaomba waendelee na moyo huo huo wa kuthamini timu yao.

Naye Meneja wa bia hiyo, George Kavishe akizungumza kwa niaba ya kiwanda hicho, alisema wamefurahishwa na kitendo hicho cha Simba kuacha shughuli zao na kutembelea kiwanda chao na kuona kazi ambazo zinafanywa na kampuni hiyo.

Alisema TBL inathamini mchango wa timu za Simba na Yanga kwa soka la Tanzania na ndio maana imekuwa ikizithamini timu hizo kwa muda mrefu huku akibainisha kuwa wataendelea kudhamini timu hizo.

Alisema timu hizo zimekuwa zikifanya mambo makubwa kwani zimekuwa zikiwapatia vijana mbalimbali ajira kwa kupitia timu zao.

Kavishe alisema kupitia kudhamini timu hizo pia wamekuwa wakijitangaza sehemu mbalimbali kwani iwapo timu ikienda kucheza nje ya nchi wanaenda kukitangaza kinywaji cha Kilimanjaro Lager.

No comments:

Post a Comment