10 August 2012
Simba kujichimbia Arusha *Kuivutia kasi Azam FC
Na Elizabeth Mayemba
MABINGWA wa Tanzania Bara Simba, leo wanatarajia kwenda jijini Arusha kwa ajili ya kuweka kambi kujiandaa na na mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC pamoja na Ligi Kuu Bara.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga alisema timu hiyo itakaa Arusha mpaka siku moja kabla ya mechi ya Ngao ya Jamii.
"Leo timu inakwenda jijini Arusha kwa ajili ya kuweka kambi, kocha ametaka kukaa pamoja na wachezaji wake kwa muda mrefu, hivyo watakaa huko na kugeuka siku moja kabla ya kuvaana na Azam FC," alisema Kamwaga.
Alisema pia Agosti 18, mwaka huu timu hiyo inatarajia kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya FC Leopards ya Kenya, mechi ya kirafiki ya kimataifa ambayo itachezwa katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Kamwaga alisema mechi hiyo itamsaidia Kocha Mkuu, Milovan Cirkovic kupanga kikosi cha kwanza kutokana na kuwa na wachezaji wengi ambao wote wana uwezo.
Pia aliwataka mashabiki wa timu hiyo wawe na imani na timu yao, kwani kufungwa mabao 3-1 na Nairobi City Stars, ndiyo njia mojawapo kwa kocha kuangalia upungufu katika kikosi chake.
"Kocha alichezesha wachezaji karibu wote kwa lengo la kuangalia mchezaji mmoja mmoja, hivyo kipigo hicho kisiwakatishe tamaa mashabiki wa timu hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment