16 August 2012
Shule za Green Acres zadaiwa kuiba umeme
Na Mariam Mziwanda
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO), limeendelea kuwanasa wateja wake ambao wanalihujumu shirika hilo kwa kuiba umeme ambapo jana Maofisa wake walibaini wizi huo katika Shule za Green Acres, katika operesheni maalumu.
Wizi huo ulibainika kuanzia katika shule ya awali, msingi na sekondari ambazo zote zinamilikiwa na Diwani wa Kata ya Magomeni, Dar es Salaam, Bw. Julian Bujugo (CCM).
Akizungumza na Majira baada ya kukata umeme katika shule hizo, Mtaalamu wa Mita, Kitengo cha Udhibiti wa Upotevu Mapato Makao Makuu ya TANESCO, Bi. Stewartness Makiko, alisema wamebaini matumizi makubwa ya umeme katika shule hizo wakati manunuzi yake ni kidogo.
Alisema mbali na matumizi hayo, pia waligundua matumizi yasiyo halali yaliyokuwa yakifanyika katika shule hizo hususan uondoaji wa fezi kuu ya umeme iliyounganishwa kwenye luku hivyo kupitisha umeme.
“Hizi shule zimefungwa mita tangu mwaka 2005, walipounganisha umeme lakini malipo yao yamekuwa ya kusuasua huku matumizi yakiwa makubwa,” alisema Bi. Makiko na kuongeza kuwa, deni la shule hizo haliwezi kujulikana kwa sasa.
Bi. Makiko alilalamikia ushirikiano mdogo alionao mmiliki wa shule hizo ambaye alikataa kusaini fomu ya ukaguzi wa TANESCO na kutokuwepo eneo la tukio pamoja na viongozi wengine.
Kwa upande wake, Meneja Uhusiano wa TANESCO Bi. Badra Masoud, alisema shirika hilo litaendelea kuwafanyia kazi wahujumu wote bila kujali nyadhifa zao.
Aliwataka wadaiwa kuhakikisha wanajisalimisha ndani ya wiki mbili kabla mpango wa kupigwa mnada nyumba zao haujawafikia.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment