16 August 2012
Dkt. Slaa kupigania ndoa yake Agosti 2
Na Rehema Mohamed
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imepanga kuanza kusikiliza pingamizi la Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Willibrod Slaa, kuhusu ndoa yake kuanzia Agosti 2 mwaka huu, baada ya mkewe Bi. Rose Kamili kufungua kesi ya zuio la ndoa mahakamani.
Mdaiwa mwingine katika kesi hiyo ni Bi. Josephine Mshumbushi ambaye ni mchumba wa Dkt. Slaa ambao wote wanawakilishwa na wakili wa kujitegemea Bw. Mutakyamilwa Philemoni.
Tarehe hiyo imepangwa jana na Jaji Laurance Kaduri, anayesikiliza shauri hilo wakati kesi hiyo ilipoletwa mahakamani hapo ili kuanza kusikilizwa na kusema kesi hiyo itasikilizwa kwa njia ya maandishi.
Jaji Kaduri alimtaka Bw. Joseph Thadayo ambaye ni wakili wa Bi. Kamili kujibu za pingamizi hilo Septemba 4 mwaka huu ambapo uwasilishwaji wa hoja za nyongeza kwa upande wa Dkt. Slaa ufanyike Septemba 13 mwaka huu.
Katika hoja zake, Dkt. Slaa anasema yeye na Bi. Kamili hawakuwa na ndoa bali dhana ya ndoa, hivyo hakupaswi kupinga ndoa yake inayotarajiwa kufungwa kisheria.
Hoja nyingine inadai Bi. Kamili hakupaswa kufungua kesi ya ndoa bali alitakiwa kuwasilisha mahakamani maombi au hati ya kiapo ya kudai kama kuna mali walizochuma pamoja au matunzo ya watoto.
Katika shauri hilo la madai ya ndoa namba 4/2012, Bi. Kamili anapinga ndoa hiyo isifungwe na kuiomba Mahakama itanganze yeye na Dkt. Slaa bado ni wanandoa na itamke kuwa ndoa yao bado ni halali na hiyo anayotarajia kuifunga ni batili.
Bi. Kamili pia anaiomba Mahakama isikubali shauri hilo lipelekwe kwenye Bodi ya Maridhiano ya Masuala ya Ndoa kwa ajili ya kupatanishwa.
Katika madai yake, Bi. Kamili ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu (CHADEMA) anadai Bi. Mshumbushi alimshawishi mumewe (Dkt. Slaa) kuivuruga ndoa yake.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment