16 August 2012
Na Magreth Kinabo, Maelezo-Dodoma
WAZIRI Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, amewataka wanafunzi wote nchini kuwa na nidhamu, kujituma, kuzingatia maelekezo ya walimu wao na kuepuka makundi ili waweze kufanya vizuri katika masomo.
Aliwataka wanafunzi waliofanya vizuri kwenye mtihani wa kuhitimu kidato cha sita mwaka huu, kuongeza juhudi zaidi ili kujiwekea msingi mzuri wa maisha.
Bw. Pinda aliyasema hayo bungeni mjini Dodoma jana kabla ya kuwatunuku vyeti wanafunzi 19 kati 20 waliofanya vizuri katika mtihani huo, kutoka shule mbalimbali nchini isipokuwa mmoja Jamal Juma ambaye yupo nje ya nchi.
Wanafunzi hao ambao wote walipata daraja la kwanza katika mtihani huo, saba kati yao wanatoka wanatoka shule ya wasichana Marian, watatu Mzumbe, wawili Fedha, wawili Kibaha ambapo shule za Kilakala, Ufundi Ifunda, Tabora girls, Tabora boys, Mpwapwa na Minaki zilitoa mwanafunzi mmoja mmoja.
“Mmefanya vizuri, mnastahili na hongereni Sana, tunataka ufaulu wenu uwe mzuri zaidi... hivi sasa ninyi mnakweda kujenga weledi, mnakuwa wataalamu wa fani fulani.
“Tumieni muda wenu kujifunza, kutafuta maarifa zaidi na kuvumbua mambo makubwa zaidi ambayo yatawasaidia ninyi wenyewe kujiletea maendeleo makubwa zaidi,” alisema Bw. Pinda.
Alisema ni vizuri utaratibu wa kuwatambua wanafunzi bora uwe endelevu na kama itawezekana, wapatiwe fursa ya kuendelezwa vyuo vikuu vya kipekee nje ya nchi hasa kwenye fani ambazo zitajenga uwezo kwa Taifa.
Bw. Pinda alisema kati ya shule 10 wanazotoka wanafunzi hao, wawili walikuwa katika shule za kata ambao ni Ester Marcel, kutoka Shule ya Sekondari ya Wasichana Olele, Kilimanjaro na Brighton Lema kutoka Shule ya Sekondari Kitangiri, jijini Mwanza.
“Napenda kuwapongeza wanafunzi hawa kwa jihudi kubwa ambazo wamezionesha, kufaulu kwao kunadhihirisha kuwa shule za kata kama tutaweka bidii, zitafanya vizuri zaidi,” alisema.
Alitoa wito kwa walimu wote nchini kushirikiana na wazazi pamoja na Serikali ili kufundisha watoto kwa bidii waweze kufanya vizuri katika masomo yao kama wanafunzi waliotunukiwa vyeti hivyo.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dkt. Shukuru Kawambwa, alisema wanafunzi hao watazawadiwa kompyuta ndogo 'Laptop', na sh. 200,000 kila mmoja.
“Shule iliyotoa mwanafunzi bora nayo itazawadiwa sh. milioni moja katika hafla maalumu itakayofanyika jioni ya leo (jana), wanafunzi 16 wanatoka katika mchepuo wa PCM, na mmoja mmoja kutoka mchepuo wa PGM, CBA, ECA na HKL,” alisema.
Spika wa Bunge, Bi. Anne Makinda aliwataka wanafunzi hao kuwa makini na makundi na kuzitaka shule nyingine kufanya juhudi ili ziweze kufanya vizuri.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment