07 August 2012
Sera ya matibabu bure kwa wazee ni kiini macho
Na Livinus Feruzi
“HAKUNA jinsi ya kukwepa uzee kila mwanadamu ni mzee mtarajiwa” huu ndio ujumbe (wosia) wa wazee kwa viongozi wenye maamuzi katika ngazi za juu serikalini kuutafakari wakati wa mipango yao.
Oktoba mosi kila mwaka wazee Tanzania huungana na wazee wenzao duniani kote kuadhimisha siku ya wazee duniani, ambapo hutumia siku hiyo kuwasilisha hoja, kero na hisia zao kwa serikali juu ya masuala mbalimbali.
Maadhimisho ya siku hii huambatana na kauli mbiu mbalimbali ambazo huwa na lengo la kuelezea masuala kadhaa yanayohusu mustakabali wao katika maisha yao ya uzeeni katika nchi husika.
Baraza kuu la umoja wa mataifa lilitenga siku hiyo maalumu ya wazee duniani likiwa na lengo la kutoa nafasi kwa mataifa mbalimbali duniani kutafakari hali ya maisha ya wazee katika mataifa yao.
Aidha baraza hilo lililenga kutoa fursa kwa kila nchi kuangalia mapungufu yaliyopo katika mipango ya taifa husika katika kushughulikia kundi hili muhimu la wazee ili kuwaboreshea maisha yao.
Siku hii hutumika kukumbusha kila mwanadamu kuwa yeye ni mzee mtarajiwa kwani uzee hakuna jinsi ya kuukwepa na hivyo kuwataka viongozi wenye maamuzi serikali kuweka mipango endelevu ya kuboresha maisha ya wazee kwa sababu hata viongozi hao muda utafika wa kuingia katika kundi la wazee.
Tafsiri ya uzee inachukuliwa kama hatua ya mwisho ya makuzi ya binadamu kuanzia utoto, ujana hadi uzee, na inatofautina kutoka nchi moja hadi nchi nyingine.
Kwa Tanzania Sera ya taifa ya afya na sheria ya utumishi wa umma inazingatia umri ya miaka 60 kuwa ndio kigezo cha uzee kwani nguvu za kufanya kazi zinakuwa zimepungua.
Aidha wazee nchini wamegawanyika katika makundi mbalimbali, ambapo lipo kundi ya wazee wastaafu, wazee wakulima, wafugaji, wavuvi na wazee wasio na ajira, makundi yote ya wazee yanatofautiana kimatatizo na kimahitaji kutoka kundi moja hadi jingine.
Hii inatokana na ukweli kwamba mzee mstaafu matatizo yake hayawezi kulinganishwa na makundi yaliyosalia kwa sababu mstaafu anapewa pensheni ambayo kwa kiasi inamsaidia kwa mahitaji ya kawaida ya kila mara.
Licha ya ukweli kwamba mzee anapozeeka nguvu za uzalishaji zinapungua, lakini kundi hili ni muhimu kwani ni hazina kubwa ya taifa kwa sababu wao ndio wamejenga misingi bora ya taifa ingawa kwa sasa wapo baadhi ya viongozi wa serikali wameanza kuharibu misingi hiyo.
Kutokana na wazee hao ndio maana tulishuhudia Tanzania ikiadhimisha miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika ikiwa kama taifa moja lenye umoja na mshikamano huku kwa kiasi fulani likiwa limefanikiwa kupiga hatua kwa baadhi ya maeneo.
Pamoja na umuhimu wa wazee hao nchini Tanzania bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo umaskini wa kipato, magonjwa nyemelezi, mabadiliko ya tabia nchi, makazi duni, malazi duni na afya duni.
Ni matatizo hayo ambayo wamepelekea baadhi ya wazee tena ambao wanaelezwa kudai na kupigania uhuru kwa sasa kuamua kuingia mitaa na kuanza kuomba kwa ajili ya kupata mahitaji yao, huku takwimu zikionyesha kwamba wazee wengi maskini wakielezwa kuishi vijijini.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na shirika la kimataifa la Help Age International takribani asilimia 90 ya wazee Tanzania ambao ni maskini wanaishi maeneo ya vijijini.
Tanzania kwa sasa inakadiriwa kuwa na idadi ya wazee milioni 2.4 ambayo ni sawa na asilimia 5.7 ya watanzania wote, ambapo hata hivyo wazee hao wanaelezwa kutunza asilimia 53 ya watoto yatima.
Bw. John Kamachale anapaza sauti ya wazee ya kuwa pamoja na agizo la serikali la matibabu bure kwa wazee, bado baadhi ya hospitali, vituo vya afya na zahanati vinawataka wazee walipie gharama za matibabu.
Anasema mbali na kulipishwa gharama za matibabu, bado wazee hao hawathaminiwi katika vituo hivyo na kuwa wanapuuzwa na baadhi ya watumishi, hali ambayo isiporekebishwa huenda ikahatarisha maisha yao.
Bw. Kamachale anasema wazee wanaishi maisha ya shida hasa kutokana na mzigo walioubeba wa kulea na kutunza watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu (wajukuu) ambao walipoteza wazazi au walezi kwa sababu ya ugonjwa wa UKIMWI.
Wanasema wakati umefika wa serikali kuwapatia vitambulisho maalumu vitakavyowawezesha kupata punguzo la gharama kwa huduma zinazotelewa kwa malipo ikiwa ni pamoja na kupata upendeleo kwenye maeneo ya msongamano wa watu.
Bw. Kamachale anasisitiza kuwa mzee kupatiwa pensheni kama haki yao ya kutambua mchango wao wa kujenga misingi imara na utawala bora kwa maendeleo ya taifa ikiwemo wazee kupewa nafasi za uwakilishi katika ngazi mbalimbali za maamuzi.
Anasema wakati umefika kwa serikali kuanza kutoa msaada wa fedha na chakula kwa wazee wanaolea na kutunza yatima ili kuwapunguzia matatizo wazee na kuongeza kuwa uzee hakuna jinsi ya kuukwepa na hivyo kuwataka viongozi wenye maamuzi serikali kutambua kwamba ni wazee watarajiwa.
Wazee hao wanatumia siku hii kuikosoa serikali kutokana na maelekezo ya kiutendaji kukinzana matamko ya kisera mathalani lengo la MKUKUTA linasema matibabu kwa wazee wote yatolewe bila malipo kwa asilimia 100 ifikapo mwaka 2010 huku sera ya taifa ya afya inasema matibabu kwa wazee bila malipo ni kwa wale wasiojiweza au maskini.
“Linalotusikitisha wazee ni kwamba licha ya serikali kutambua umuhimu wetu, bado maelekezo yake ya kiutendaji yanakinzana na matamko yake ya kisera mathalani lengo la MKUKUTA na sera ya taifa ya afya hivyo sasa tunaomba tamko la serikali juu huduma ya matibabu bure kwa wazee” wanasema wazee hao.
Wanasema malengo ya MKUKUTA ya kuboresha huduma kwa wazee yaliyotakiwa kuisha mwaka 2010 bado hayajafikiwa na hivyo kuitaka serikali itilie mkazo ili kufikia malengo hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yatasaidia kuboresha maisha ya wazee.
Wanasema bila Dkt. Kurt Madoern raia wa Uswizi ambaye aliamua kutumia pensheni yake ya kustaafu kusaidia wazee wilayani humo, huenda maisha yao yangekuwa magumu zaidi ya ilivyo sasa.
Akizungumza kwa niaba ya shirika la kwa wazee Nshamba Ofisa kutoka shirika hilo Bi. Revina Jonas anasema mwaka 2003 baada ya Dkt. Kurt kustaafu alianza kutumia sehemu ya pensheni kuwasaidia wazee waliokuwa wakimjia na kumuomba msaada.
Anasema wazee hao walikuwa wanaomba gharama za matibabu, chakula, karo na michango mingine ya shule kwa wajukuu wao na kuwa huo ndio ulikuwa mwanzo wa shirika hilo, ambapo wakati huo alikuwa akiwapatia pensheni ya shilingi 3,000 wakiwa wazee 54.
Bi. Jonas anasema kwa sasa pensheni shirika linahudumia jumla ya wazee 984 tu na wajukuu wao 585 kutoka kata sita, ambapo kila mzee anapatiwa pensheni ya shilingi 10,500 kwa mwezi huku pia kila mjukuu akipewa shilingi 6,000.
Anafafanua kuwa mbali na kuwapatia pensheni hizo pia baadhi ya wazee hao wamepatiwa mahitaji mengine ikiwa ni pamoja na kuwajenga nyumba 53, matanki ya maji na kuwajengea miradi kadhaa ikiwemo ya kilimo na ufugaji kwa kuwapatia mbuzi.
Bi Jonas anasema pamoja na jitihada hizo za kuwakomboa wazee changamoto kubwa ni kuwa idadi ya wazee wanaohitaji msaada ni kubwa, ambapo inaongezeka kila mara kulinganisha uwezo wa shirika.
Hata hivyo kutokana na pensheni hiyo ambayo imetolewa kwa baadhi ya wazee wilayani Muleba, takwimu zilizotolewa na shirika la help age international zinaonyesha asilimia 57 waliopewa pensheni wameachaa kuombaomba kulinganisha na 2/3 ya wazee hawakupewa pensheni wanaoendelea kuombaomba.
Aidha takwimu hizo zinaonyesha kwamba asilimia 22 wa wazee waliopatiwa pensheni hiyo walilalamikia kuumwa mara kwa mara tofauti na asilimia 37 wasiopewa pensheni waliolalamikia kuumwa mara kwa mara.
Kwa mujibu wa takwimu hizo watoto ambao kaya zao wanapata pensheni licha ya kupata chakula kizuri pia wanapata sabuni ya kuwawezesha kufua na kuoga, ambapo pia mahudhurio yao shuleni ni mazuri kulinganisha na wasiopata pesheni.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
am supporting elders role in community ...thank you for document
ReplyDeleteThis paragraph gives clear idea designed for the new viewers of
ReplyDeleteblogging, that actually how to do running a blog.