17 August 2012

Sakata la rushwa wabunge njia panda *Ni wale wa Kamati ya Madini iliyovunjwa



Na Benedict Kaguo, Dodoma

SAKATA ya rushwa kwa baadhi ya wabunge, limewaweka njia panda wajumbe waliokuwa kwenye Kamati ya Nishati na Madini baada ya kamati iliyopewa jukumu la kuchunguza tuhuma dhidi yao, kushindwa kutoa matokeo ya uchunguzi wake licha ya muda waliopewa siku 14, kumalizika jana.

Kamati hiyo ya Nishati na Madini ilivunjwa na Spika wa Bunge Bi. Anne Makinda ili kupisha uchunguzi kutokana na tuhuma za baadhi ya wajumbe wake kuhusika na vitendo vya rushwa.

Kutokana na tuhuma hizo, Bi. Makinda aliunda kamati ndogo ya wabunge wanne chini ya Mwenyekiti wake, Brigedia Jenerali mstaafu Hassan Ngwilizi ili kuchunguza tuhuma hizo kama zina ukweli wowote.

Wajumbe wengine wa kamati hiyo ni Mbunge wa Manyoni
Mashariki Kapteni mstaafu, John Chiligati (CCM), Mbunge wa Karagwe Bw. Gosbert Blandes (CCM), Mbunge Viti Maalumu, Bi. Riziki Omari Juma (CUF) na Mbunge wa Mpanda Mjini Bw. Saidi Amour Arfi (CHADEMA).

Wakizungumza na Majira katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma jana, baadhi ya wabunge na waliokuwa wajumbe wa kamati hiyo iliyovunjwa, walisema muda uliotolewa kwa kamati hiyo kufanya uchunguzi wake siku 14, umemalizika jana.

Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ambaye hakutaja jina lake liandikwe gazetini, kitendo cha ripoti hiyo kutotolewa kwa muda muafaka kutawaweka njia panda wabunge hasa kwa wapiga kura wanaporudi majimboni mwao.

“Kamati hii ilipewa siku 14 iwe imetoa ripoti, siku zimekwisha lakini haikufanya hivyo kabla hatujaenda majimboni ili wapiga kura wajue ukweli, ni vizuri ikatoa taarifa ili tukifika jimboni kusiulizwe maswali na wananchi vinginevyo watatuweka njia panda,” alisema.

Aliongeza kuwa, licha ya kwamba si wajumbe wote ambao wametuhumiwa kwa rushwa, lakini kitendo cha kamati nzima kuvunjwa na Spika kimezusha maswali mengi kwa wapiga kuwa.

“Ndio maana tunataka ripoti hii isomwe mapema ili wananchi waweze kujua ukweli wa tuhuma hizi,” alisema.

Wajumbe wa kamati hiyo ambayo iliyovunjwa ni pamona na Bw. Seleman Zedi (Mwenyekiti), Bi. Diana Chilolo (Makamu Mwenyekiti) ambapo wajumbe ni Bw. Yusuph Haji Khamisi, Bi. Mariam Kisangi, Bi. Catherine Magige, Abia Nyabakari na Bw. Charles Mwijage.

Wengine Bw. Yusuph Nassir, Bw. Christopher Ole Sendeka, Dkt. Festus Limbu, Shafin Sumar, Mhandisi Athumani Mfutakamba, Bi. Lucy Mayenga, Bi. Josephine Chagulla, Mwanamrisho Taratibu Abama, Bw. David Silinde, Bw. Selemani Nchambis, Kisyeri Chambiri, Bw. Ali Mbaruk Salim, Bi. Sarah Msafiri, Munde Abdalah Tambwe, Bi. Vicky Kamata na Bw. John Mnyika.

Akizunguma na Majira kuhusu tuhuma za rushwa kwa baadhi ya wabunge, Naibu Spika wa Bunge, Bw. Job Ndugai, alisema ni vyema wananchi wakawa na subira hadi Kamati ya Maadili iliyopewa jukumu hilo itakapowasirisha ripoti yake.

“Wananchi wawe na subira, kamati hii imepewa kazi nzito ya kuthibitisha tuhuma ili ukweli uweze kujulikana,” alisema.


3 comments:

  1. IWAPO KAMATI IMEONGEZEWA MUDA HADI SEPTEMBA 11 SI VEMA KULIZUNGUMZIA SUALA HILI NJE YA BUNGE NI KUCHOCHEA VURUGU KUOMBA HURUMA MTU ASIZOSTAHILI UKWELI UKIDHIHIRIKA UONGO HUJITENGA

    ReplyDelete