07 August 2012

Rupia, Binda 'wakaliwa kooni' Jangwani



Na Amina Athumani

WANACHAMA wa Klabu ya Yanga wameanzisha vurugu ya kuwazuia Wajumbe wa Klabu hiyo, Said Rupia, Mohamed Binda na Tito Osoro kuingia kwenye ukumbi wa klabu hiyo katika sherehe za kusimikwa na kuapishwa kwa viongozi wa klabu hiyo.


Akizungumza kwa niaba ya wanachama wenzake Makao Makuu ya Klabu hiyo Mitaa ya Twiga na Jangwani Dar es Salaam jana, Mwanachama Said Motisha (0074), alidai wajumbe hao ndio watakaouvuruga uongozi wa Yanga chini ya Mwenyekiti wake Yusuf Manji.

Alidai klabu itaingia kwenye mzozo mkubwa kutokana na wajumbe hao kuwa ni wanafki na kamwe hawana mapenzi mema na klabu hiyo.

"Huwezi kuchukua tenga la samaki wazuri ukawachanganya na samaki wabovu kwani watanuka tenga zima, hivyo tunasema hawa hatuwataki watauharibu uongozi wa Manji,"alisisitiza Motisha.

Alisema wajumbe hao wasingekuwepo klabuni hapo na kwamba wameamua kutuliza jazba zao kutokana na kumuheshimu Mlezi wa klabu hiyo, Mama Fatma Karume aliyekuwa mgeni rasmi katika shughuli hiyo.

"Hawa salama yao ni kwa sababu ya Mama Karume lakini hapa wasingekaa kabisa kwa sababu hakuna mwanachama hata mmoja anayewataka,"alisema Motisha.

Wanachama wa klabu hiyo kutoka matawi mbalimbali wameungana pamoja jana katika sherehe za kuapishwa kwa viongozi wao wapya ambao ni Mwenyekiti Yusuph  Manji, Makamu Mwenyekiti, Clementi Sanga na wajumbe Aron Nyanda, George Manyama na Mussa Matabaro.

No comments:

Post a Comment