31 August 2012

Ngulume afariki dunia




Stella Aron na Heri Shaaban

MWANASIASA mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya mbalimbali nchini kwa miaka 18, Bi. Hawa Ngulume, amefariki dunia jana asubuhi jijini Dar es Salaam.


Kutokana na msiba huo, Rais Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu na kusisitiza kuwa, enzi ya uhai wake, alikuwa kiongozi shupavu aliyesimamia kidete kusimamia maamuzi yake katika majukumu muhimu ya kitaifa ili kuwaletea wananchi maendeleo.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, ilisema Rais Kikwete ameitaka familia yake kuwa na moyo wa uvumilivu na ujasiri wakati huu wa maombolezo ya msiba huo.

“Nilimfahamu marehemu kama kiongozi shupavu aliyesimamia kikamilifu maamuzi yake hivyo kuthibitisha ukweli kwamba, wanawake wakipewa fursa wanaweza.

“Familia yake imeondokewa na mhimili muhimu na kiongozi wa familia, natambua machungu mliyo nayo hivi sasa, nawahakikishia niko pamoja nanyi kuomboleza msiba huu mkubwa,” alisema Rais Kikwete na kuongeza kuwa, Mwenyezi Mungu aipokee na kuilaza mahala pema peponi roho ya marehemu, Amina. 

Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Bw. Jordan Rugimbana, alisema marehemu alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya saratani na kichomi kwa kipindi kirefu ambapo mauti yamemkuta akiwa Hospitali ya Lugalo, Dar es Salaam.

Alisema kifo chake ni pigo kubwa kwa familia yake na Taifa kwani enzi za uhai wake, alikuwa mchapa kazi hodari na mwenye ujasiri mkubwa sifa ambazo zilimwezesha kushika nafasi za uongozi.

Bw. Rugimbana alisema taratibu za mazishi zinafanyika nyumbani kwake Goba Kinzudi. Kabla ya kifo chake, marehemu aliwahi kutibiwa katika hospitali mbalimbali ikiwamo ya Ocean Road pamoja na kupelekwa nchini India.
 
Miongoni mwa Wilaya alizowahi kuziongoza kama Mkuu wa Wilaya ni pamoja na Kinondoni (Dar es Salaam), Kibaha, Kondoa, Bagamoyo (Mkoa wa Pwani), Singida na Mbarali (Mbeya), ambako ndiko alistaafu mwaka 2010.

Hata hivyo, wakati gazeti hili likienda mitamboni, kulikuwa na taarifa zisizo rasmi kuwa marehemu anatarajiwa kusafirishwa leo kwenda Singida kwa ajili ya mazishi. Taarifa nyingine zinadai anazikwa leo jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment