28 August 2012


Na Rehema Mohamed

BARAZA la Vyuo Vikuu Afrika Mashariki (IUCEA), limesema kuwepo ulinganifu wa elimu zinazotolewa katika vyuo vikuu vya nchi hizo, utawezesha wahitimu wa vyuo hivyo kupata kazi kwa unafuu katika nchi zote za Afrika Mashariki.

Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Profesa Mayunga Nkunya, aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika mkutano wa wadau wa vyuo vikuu vya nchi hizo.

Alisema lengo la mkutano huo ni kujadili na kuweka viwango vinavyofanana vya elimu zinazotolewa katika vyuo husika ambapo hivi sasa wameanza na masomo ya biashara.

Aliongeza kuwa, maandalizi ya ulinganifu huo katika utoaji elimu ulianza mwaka 2006 na tayari vyuo vipatavyo 47 kati ya 91, vilivyopo katika nchi hizo, vimeshanza programu hiyo.

“Tupo katika hatua ya ulinganishaji mitaala, tumeanza na somo la biashara ambalo karibu vyuo vingi vikuu vinafundisha somo hili na tutafuatia pamoja na somo la Habari na Teknolojia ya Mawasiliano (IT).

“Suala la kuzingatia ni kuona kuwa mitaala inayotungwa inalenga matarajio ya mhitimu wa chuo husika ili soko la pamoja litakapofunguliwa, waweze kupata ajira katika nchi zote za Afrika Mashariki,” alisema Prof. Nkunya.

No comments:

Post a Comment