28 August 2012
Askari wanyamapori wadaiwa kupora fedha zaidi ya mil. 4/-
Na Said Njuki, aliyekuwa Kondoa
WAFANYABIASHARA watatu wakazi wa Kijiji cha Itolwa, Wilaya ya Kondoa, mkoani Dodoma, wameiomba Serikali kuwasaka na kuwachukulia hatua za kisheria askari sita wa Pori la Akiba Mkungunero, kwa madai ya kuwateka, kuwatesa pamoja na kuwapora zaidi ya sh. milioni nne.
Habari zilizolifikia gazeti hili ambazo zimethibitishwa na mmiliki wa gari lililotekwa, Bw. Rajabu Iddi, zilisema tukio hilo limetokea alfajiri ya Agosti 23 mwaka huu, katika eneo la Kimotoro.
Inaelezwa kuwa, askari hao wakiwa na gari yao aina ya Land Rover, rangi ya kijani, waliwasimamisha wafanyabiashara hao wakati wakitokea Mjini Arusha na kuomba wapatiwe mirungi.
“Baada ya kutuomba mirungi, sisi tuliwajibu kuwa katika gari yetu hatuna bidhaa hiyo, majibu yetu yalizua malumbano kidogo lakini hawa askari walichukua bunduki na kupiga risasi gurudumu la gari lenye namba za usajili T 955 AJJ, aina ya Isuzu Injection.
“Mbali ya kufanya hivyo, pia walitushusha katika gari kupitia madirishani na kuanza kutupiga, wengine kupekuliwa mifukoni na kuchukuliwa fedha zao ambazo zilitokaana na mauzo ya mahindi,” alisema mfanyabiashara huyo (jina limehifadhiwa).
Alidai kuwa, baada ya askari hao kukamilisha azma hiyo, walitoa onyo na kuwataka wasipeleke taarifa za tukio hilo kituo chochote cha Polisi na kama watafanya hivyo, watajuta kuzaliwa.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu akiwa katika pori hilo, dereva wa gari hiyo Bw. Francis Pele, kwa jina maarufu 'White', alidai wameshindwa kutoa taaarifa polisi wakihofia kupigwa risasi kutokana na onyo walilopewa na askari hao.
“Katika gari nilikuwa na wenzangu wawili mmoja anaitwa Bw. Shaban Idonge, tukio hili lilitokea alfajiri lakini vitendo hivi vimekuwa vikijirudia mara kwa mara.
“Hali hii husabbisha hofu kwa kwa wasafiri na wasafirishaji mazao ambao wanatumia barabara hii kwenda na kurudi kutoka Arusha, hivyo kulazimika kupitia barabara ya Arusha Babati hivyo kusababisha uongezeko la gharama kutokana na umbali.
“Ukitaka kupitia barabara hii ujiandaye kupigwa hata kuporwa kila kitu ulichonacho, mimi naamini kila kitu kina mwisho, tunaiomba Serikali kupitia Jeshi la Polisi watusaidie,” alisema.
Meneja wa pori hilo Bw. Ernest Madanya, juzi alithibitisha kwa njia ya simu kuwepo askari wa doria katika eneo hilo ambao gari lao liliharibika Alhamisi jioni ambapo Ijumaa, alituma gari nyingine na fundi lakini gari hilo lilishindikana kupona hivyo liliachwa porini.
“Ni kweli askari wa doria walikuwa huko, hivi ninavyozungumza bado sijaonana nao kwani walirudi usiku wa manane, nimepata taarifa za tukio hili kutoka Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kondoa (OCD), nakuhakikishia tutalifanyia kazi kikamilifu.
“Sisi hatupo kazini kwa ajili ya kunyanyasa wananchi wasio na hatia,” alisema Bw. Madanya mwishoni mwa wiki.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment