28 August 2012

Mwanafunzi mbaroni kwa kupinga sensa


Na Anneth Kagenda

JESHI la Polisi nchini linamshikilia mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Bw. Yusuf Ernest, mkazi wa Mbagala, Dar es Salaam kwa tuhuma za kusambaza ujumbe kwenye simu za mkononi ili kuhamasisha wananchi wasijitokeze kuhesabiwa katika Sensa ya Watu na Makazi iliyoanza Agosti 26 mwaka huu.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Sadick Meck Sadik, aliyasema hayo jana baada ya kumaliza mazungumzo yake na  wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa iliyokuwa ikijadili ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Alisema mbali ya mwanafunzi huyo kukutwa na ujumbe huo, jeshi hilo pia linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kuhamasisha wananchi wasishiriki sensa.

“Kati ya watyuhumiwa hawa, wawili wanatoka katika Wilaya ya Temeke na wengine Kinondoni, ambao walikutwa wakihamasisha waananchi wasishiriki sensa kwa sababu wanazojua wao, mwingine alikataa kuhesabiwa jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

“Kimsingi sensa inakwenda vizuri lakini katika mchakato huu, baadhi ya watu wamekwenda kinyume na sheria kwa kukataa kuhesabiwa hivyo hatuwezi kuwavumilia,” alisema.

Alisema zaidi ya Waislamu 20 walikuwa wamejifungia katika Msikiti maarufu wa Masjd Simba, uliopo Mbagala Maji Matitu wakidai mchakato huo ukimalizika watatoka.

“Kwa juhudi zetu tumeweza kuwaelimisha na wameelewa umuhimu wa sensa hivyo wameenda kuungana na wenzao ili wahesabiwe, katika baadhi ya maeneo kama ya Kagera na Magomeni, kuna watu waliwazuia wenzao wasihesabiwe,” alisema.

Bw. Sadik alisema kama kutakuwa na watu ambao wanajifungia ili wasihesabiwe au kukimbilia mikoani, sheria haitosita kuchukua mkondo kwani ni kosa la jinai.

“Kukimbia hakusaidii chochote, tumeweka makarani kila eneo hadi Kituo cha Mabasi yaendayo mikoani Ubungo, hivyo isiwe kisingizio cha kutohesabiwa hakipo,” alisema.


No comments:

Post a Comment