16 August 2012

Mtanda ashinda Ubunge wa Afrika



Na Benedict Kaguo, Dodoma

MBUNGE wa Mchinga, mkoani Lindi, Bw. Said Mtanda (CCM), ameibuka mshindi katika kinyang'anyilo cha kuwania nafasi ya ubunge wa Bunge la Afrika.

Katika uchaguzi huo, uliofanyika bungeni mjini Dodoma jana, Bw. Mtanda alimshinda Mbunge wa Nzega, mkoani Tabora, Dkt. Hamisi Kigwangalla (CCM).

Bw. Mtanda ameziba nafasi iliyoachwa wazi na Mbunge wa Shinyanga mjini, Bw. Stephen Masele aliyeteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, Msimamizi wa Uchaguzi ambaye pia ni Katibu wa Bunge, Dkt. Thomas Kashililah, alisema Bw. Mtanda alipata kura 145 dhidi ya 72 za Dkt. Kigwangallah.

Wabunge hao walijieleza mbele ya wabunge kwa dakika tatu kila mmoja wakitumia lugha ya Kiingereza ambapo baadae kila mmoja aliulizwa maswali matatu.

Uchaguzi huo ambao ulishirikisha wabunge wa CCM pekee, ulitawala na kampeni kali za wagombea kila mmoja akiwaomba wabunge wamuunge mkono ili kupata ushindi.

Baada ya kutangazwa mshindi, Bw. Mtanda aliwashukuru wabunge kwa kura walizompa ili kuiwakilisha nchi katika Bunge la Afrika ambapo ushindi huo ni kielelezo cha kuaminika.

“Jambo ambalo nalitegemea ni ushirikiano mkubwa kutoka kwa wabunge wenzangu ili niweze kufanikisha azma ya kuipigania nchi yangu kupitia bunge hili,” alisema.

Kwa upande wake, Dkt. Kigwangalla aliwashukuru wabunge waliompigia kura na kuahidi kuendeleza ushirikiano katika kutekeleza majukumu ya kitaifa nay a kimataifa.

No comments:

Post a Comment