16 August 2012
SAKATA LA UTOROSHAJI WANYAMA YAMETIMIA *Mkurugenzi Wanyamapori atimuliwa kazi *Sita wapewa onyo, mmoja ashushwa cheo
Na Benedict Kaguo, Dodoma
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, amemfukuza kazi Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Bw. Obeid Mbangwa na watumishi wengine wawili Bw. Simon Gwera pamoja na Bw. Frank Mremi.
Bw. Gwera na Bw. Mremi wote walikuwa watumishi wa Ofisi ya Uwindaji wa Kitalii-CITES na Utalii wa Picha mjini Arusha.
Balozi Kagasheki pia amemvua cheo aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi, Bw. Bonaventura Midala.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Balozi Kagasheki alisema uamuzi wa kuwafukuza kazi watumishi hao na kumshusha cheo Bw. Midala, umetokana na kashfa ya utoroshwaji wanyapori hai kutika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa KIA, mkoani Kilimanjaro na kusababisha hasara kubwa kwa Taifa.
Alisema wakati tukio hilo linatokea, Bw. Midala alikuwa Mkurugenzi Msaidizi sehemu ya kuzuia ujangili.
Aliongeza kuwa, Wizara hiyo pia imewachukulia hatua za kinidhamu watumishi wengine sita baada ya uchunguzi wa tuhuma zilizokuwa zikiwakabili kukamilika tangu kuibuliwa ufisadi huo na Kamati ya Bunge ya Maliasili na Mazingira pamoja na taarifa nyingine za vyombo vya habari likiwemo gazeti hili.
“Kitendo kilichofanywa na watumishi ambao tumewafukuza kazi ni makosa ya jinai na suala hili, halitaishia hapa bali tutawafikisha katika vyombo vya sheria,” alisema Balozi Kagasheki.
Aliwataja Maofisa Wanyamapori Daraja la II, ambao walitekeleza maelekezo ya Wakuu wao kinyume cha sheria na kupewa onyo kali la maandishi kuwa ni pamoja na Bi. Martha Msemo (Ofisa Leseni, Ofisi ya Uwindaji wa Kitalii-CITES na Utalii wa Picha Arusha).
Wengine Bi. Anthonia Anthony (Ofisa Leseni, Ofisi ya Uwindaji wa Kitalii-CITES na Utalii wa Picha Dar es Salaam na Bw. Silvanus Okudo (Mkuu wa Kituo cha Uwindaji wa Kitalii-CITES na Utalii wa Picha Arusha), ambaye alikiuka utumishi wake kwa kukiuka sheria na kutoa vibali.
“Maofisa wengine ambao uchunguzi dhidi yao unaendelea ni pamoja na Bw. Mohamed Madehele (Ofisi ya Matumizi Endelevu ya Wanyamapori), Bi. Mariam Nyallu (Kituo cha Uwindaji wa Kitalii- CITES na Utalii wa Picha Arusha),” alisema.
Balozi Kagasheki alikiri kuwa ndani ya Wizara hiyo kuna mitandao ya majangili ambapo taarifa za mitandao hiyo zimeanza kufahamika ambapo mapambano ili kuhakikisha rasilimali zilizopo zinawanufaisha wazawa.
Akizungumzia sakata la wanyama kupelekwa Doha na Ndege ya Qatar, alisema tayari Serikali iliwasiliana na Serikali ya Qatar lakini wamekuwa kimya kutoa ushirikiano.
“Suala la Bodi ya Hifadhi ya Ngorongoro ambayo kwa muda
mrefu imekuwa ikilalamikiwa na wabunge ni kweli ina tatizo ambalo linachangiwa na mifumo ya utumishi ndani ya bodi.
“Kama ingekuwa ni maamuzi yangu, tayari ningechukua hatua kwani hata nilipokwenda kuzungumza na wafanyakazi, walisema wazi kuwa mimi ndiye Waziri wa kwanza kwenda kuzungumza nao,” alisema Balozi Kagasheki.
Aliongeza kuwa, Mkurugenzi wa Bodi alichaguliwa wakati amefunguliwa kesi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na kusisitiza umuhimu wa wananchi kushirikiana nna Wizara ili kutokomeza vitendo vya ufisadi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment