31 August 2012
Mshindi BSS kuzindua albamu Uwanja wa Fisi
Na Mwandishi Wetu
MSHINDI wa mashindano ya Bongo Star Search (BSS) 2009, Pascal Cassian anatarajia kuzindua albamu yake ya nyimbo za injili ya Yasamehe Bure keshokutwa Uwanja wa Fisi.
Albamu hiyo itakuwa na nyimbo za Chuki ya Nini, Nikumbuke na Mimi, Jina la Yesu, Mafuriko, Pesa, Baba na Usilie.
Akizungumzia albamu hiyo alisema ina lenga kuwarudisha waliopotea kwa Mungu kwa kuwapatia ujumbe wa neno la Mungu kwa njia ya nyimbo za injili.
Alisema akiwa kama kijana ameamua kutumia muda, nguvu na akili zake nyingi katika kumwimbia na kumsifia Mungu na hivyo ametaka kuwafikishia vijana, watoto na watu wazima ujumbe kupitia nyimbo hizo.
Pia akizungumzia sababu ya kuzindulia albam yake katika eneo la Uwanja wa Fisi, alisema kutokana na sifa mbaya ya eneo hilo ameamua ambalo limekuwa likifahamika kama uwanja wa dhambi kutokana matukio mbalimbali, ambayo yanafanyika mahali hapo.
Alisema mgeni rasmi anatarajia kuwa Jaji Mkuu wa mashindano ya Epiq Bongo Star Search (EBSS), Ritha Paulsen ambaye ndiye aliyeibua kipaji chake kupitia mwaka 2009 wakati yakiitwa BSS.
Uzinduzi huo pia utasindikizwa na waimbaji wengine ambao ni Martha Mwaipaja, Sifa John, Joseph Kaka, Beatrice na wengineo wengi.
Albamu hiyo ambayo ameirekodia katika studio mbalimbali, imemchukua miezi minne kuiandaa ambapo itauzwa kwa sh. 10,000.
“Mimi kwanza nina mshukuru Mungu kwa kuniongoza mpaka kufikia hatua hii ya kuzindua albamu yangu na ameweza kunifikisha hapa kupitia programu ya BSS.
"Ndiyo nilionekana uwezo wangu wa kuimba na kushinda na kumbe ilikuwa ndiyo mwanzo wa safari yangu ya kumtumikia Mungu,” alisema Cassian.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment