02 August 2012

Mkapa awaonya wanachama EAC


Mariam Mizwanda na Tumaini Maduhu

RAIS Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Bw. Benjamin Mkapa, amezitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kuendelea kuukata mkataba wa ushirikiano kiuchumi kati ya jumuiya hiyo na Jumuiya ya Ulaya (EPA), kwani una lengo la kuua uchumi wa nchi hizo.

Bw. Mkapa aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika maadhimisho ya Siku ya Sekta Binafsi na kusisitiza kuwa, Jumuiya ya Ulaya ingekuwa na mapenzi mema na Afrika Mashariki, ingeondoa masharti magumu yaliyopo katika mkataba huo.

“Hakuna utofauti wowote kati ya mwananchi wa kawaida wa Kenya na Tanzania katika uhalisia wa maisha yao, mwananchi huyu anaweza kufanya biashara ya soko moja na mwananchi wa Ulaya tena kwa masharti,” alihoji Bw. Mkapa.

Aliongeza kuwa, hakuna sababu ya nchi za Afrika Mashariki kutumia udhaifu walionao kama nchi zinazoendelea kuyanufaisha matafa tajiri kwani nchi za Kiafrika kupitia Mawaziri wa Biashara na Viwanda, bado wamedhamiria kuwapo biashara yenye tija.

Alitumia fursa hiyo kuwataka Watanzania kuuogopa mkataba huo kwani kuingia kwao katika soko moja la biashara, kutasababisha ufirisi wa viwanda vya ndani hivyo nchi hizo kuwa tegemezi.

Alisema mkataba huo utakua na nia njema kama utalenga uwepo wa biashara yenye soko moja na mashariti nafuu na kuongeza kuwa, changamoto zilizopo katika mkataba huo zinazoweza kukwamisha nchi hizo kuendelea katika biashara ni pamoja na uwepo wa sheria inayotaka jumuiya hizo kuondoa kodi kwa nchi wanachama katika bidhaa lakini kuwapo kwa sheria ya matumizi ya bidhaa halisi.

Bw. Mkapa alishauri ndani ya mazungumzao ya mkataba huo ambayo yanaendelea, Jumuiya ya Ulaya ikubali kwanza kusaidia nchi za Afrika Mashariki kuendelea kiuchumi ili iweze kuwa na fursa sawa katika soko la viwanda.

Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Abdallah Kigoda, alisema utayari wa sekta binafsi katika kuzungumza na Sekta ya Umma ni mchango mkubwa wa kuishauri Serikali kuchangia ukuaji wa uchumi nchini.

No comments:

Post a Comment