02 August 2012

Bonite kupeleka washangiliaji London Olimpiki 2012


Na Mwandishi Wetu, Moshi

KAMPUNI  ya vinywaji baridi jamii ya Coca-Cola ya Bonite Moshi jana iliwazawadia washindi 11 wa promosheni ya Bamba tiketi ya London Olimpiki 2012 na Coca-Cola, ikiwa ni pamoja na washindi wawili ambao wamebahatika kupata tiketi za kwenda London Uingereza kushuhudia michezo ya Olimpiki. 

Washindi wengine tisa walijinyakulia majokofu ya kisasa ya milango miwili, runinga kubwa za inchi 32 na music system, tukio la kukabidhi zawadi hizo lilifanyika jana katika kiwanda cha Bonite Bottlers mjini Moshi.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kukabidhi zawadi hizo, Meneja Masoko wa Bonite Bottlers Christopher Loiruk aliwashukuru wateja wake walioshiriki katika shindano hilo na kuwatakia safari njema watakaosafiri kwenda London.

Aliwataja washindi wa tiketi ambao pia watagharamiwa chakula na malazi kuwa ni Bashir Mdee wa Kilimanjaro Polisi Mess, mkazi wa Moshi na Cuthbert Temba wa CET Garden mkazi wa Arusha.

Washindi wa majokofu ni Adrian Mushi (Moshi) John Swai (Arusha) na Edward Mallya (Singida). Washindi wa runinga ni Frank Mushi (Moshi), Beaty Tarimo (Mang’ola), Lelia Mboya (Arusha). Washindi wa Music system ni Paul Njuu (Moshi) na Robert Kamnde (Arusha) na Kastuli Erro (Karatu).

Shindano la Bamba tiketi ya London Olimpiki 2012 na Coca-Cola lilizinduliwa Mei 21, mwaka huu na kumalizika Juni 30, mwaka huu na kushirikisha wanachama wa VIP Coca-Cola Club. Washiriki walitakiwa kununua soda za kujaza friji mara nne, kuwa na ongezeko la mauzo ikilinganishwa na kipindi kama hicho cha mwaka jana, kigezo kingine kilikuwa ni kuwa na mpangilio mzuri wa soda.

Shindano hilo lililenga maeneo ambayo Bonite Bottlers inasambaza bidhaa zake, maeneo hayo ni Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Singida.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa tiketi yake, Bw Bashir Mdee (38), mmiliki wa Kilimanjaro Police Mess iliyopo mjini Moshi ameuelezea ushindi wake kuwa ni bahati ya pekee katika maisha yake.

“Nimefarijika sana kupata fursa hii ya kwenda kushuhudia michezo ya Olimpiki jijini London, Uingereza”, alisema Mdee na kuipongeza Bonite Bottlers Ltd kwa ubunifu huo.   

Michuano ya Olimpiki, ambayo hufanyika kila baada ya miaka minne imekuwa ikidhamaniwa na kampuni ya Coca-Cola tangu mwaka 1928.

No comments:

Post a Comment