29 August 2012
Michuano ya Tusker 'kutumbua' dola 450,000
Na Zahoro Mlanzi
KAMPUNI ya Bia Afrika Mashariki (EABL), imedhamini mashindano ya Kombe la Tusker kwa dola 450,000 yatakayofanyika nchini Uganda kuanzia Novemba 24 mpaka Desemba 8.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicolas Musonye ilieleza kwamba uzinduzi wa mashindano hayo ulifanyika jana Kampala, Uganda ambapo mashindano hayo yatafanyikia.
Mwaka jana mashindano hayo yalifanyika jijini Dar es Salaam ambapo timu ya Taifa ya Uganda 'The cranes' ilitwaa ubingwa baada ya kuifunga Rwanda 'Amavubi' kwa mikwaju ya penalti 4-3, baada ya kumaliza dakika 90 zikiwa zimefungana mabao 2-2 na zikaongezwa dakika 30 pia hazikufungana.
Musonye ambaye alitua jijini humo tangu juzi, alisema mechi ya kwanza itapigwa kwenye Uwanja wa Mandela mjini Namboole huku maandalizi mengine yakiendelea na kuishukuru kampuni hiyo kwa kuendelea kudhamini mashindano hayo.
Musonye alisema udhamini huo utahusisha malazi na usafiri wa ndege na mambo mengine, ambapo kati ya fedha hizo dola 60,000 zitatumika kwa zawadi ambapo bingwa atapata dola 30,000, wa pili dola 20,000 na wa tatu ni dola 10,000 na kwamba mechi zote zitarushwa hewani na Super Sport.
Alisema Shirikisho la Mpira wa Miguu la Uganda (FUFA), tayari imeshaunda Kamati Maalumu kwa ajili ya maandalizi ya mashindano hayo na kuongeza kwamba baadaye alikuwa na ahadi ya kuonana na Waziri wa Michezo wa nchini humo, Charles Bakabulindi kwa mazungumzo zaidi juu ya mashindano hayo.
Naye Mkurugenzi wa Masoko wa kampuni hiyo, Lemmy Mutahi alisema lengo lao ni kuhakikisha timu za Ukanda wa Afrika Mashariki, unakuwa na uwezo wa kucheza Kombe la Dunia 2014 litakalofanyika nchini Brazil.
Alisema wana furaha mashindano hayo kufanyikia nchini humo na kwamba udhamini wao kwa mwaka huu umeongezeka kwa asilimia tano ikilinganishwa na mwaka jana.
Mkurugenzi huyo alisema kampuni yake itaendelea kudhamini mashindano hayo kwa muda mrefu, hasa baada ya kuridhishwa na mafanikio katika mashindano yaliyofanyika mwaka jana nchini .
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment