22 August 2012

Mechi ya Simba, Azam yasogezwa


Na Mwandishi Wetu

MECHI ya Ngao ya Jamii iliyopangwa kufanyika Agosti 24, mwaka huu kati ya mabingwa wa Ligi Kuu Bara, timu za Simba na Azam FC imesogezwa mbele mpaka wiki moja kabla ya ligi haijaanza.


Hatua hiyo imetokana na ligi hiyo kusogezwa mbele kutoka Septemba Mosi na kutarajiwa kuanza Septemba 15, mwaka kutokana na kutokamilika kwa mazungumzo baina ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na wadhamini, Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom.

Akilitolea ufafanuzi suala la udhamini wa ligi hiyo, Katibu Mkuu wa shirikisho hilo Angetile Osiah, alisema baada ya kikao cha TFF na viongozi wa klabu za Ligi Kuu kilichofanyika juzi, wamekubalina mambo mbalimbali likiwemo ligi kusogezwa mbele.

"Katika kikao ilionekana kuwa kutokana na kutokamilika kwa mazungumzo hayo, mwanzo wa Ligi Kuu unatarajiwa kuwa Septemba 15, mwaka huu na hii inatokana na ukweli kwamba mazungumzo hayo
yanatarajia kukamilika mwishoni mwa wiki hii kwa kuwa yameshafikia hatua nzuri," alisema Osiah.

Alisema kutokana na mwenendo wa hali halisi ya mazungumzo hayo, mkataba unaweza kusainiwa wakati wowote, baada ya kukamilika kwa mazungumzo hayo.

Katibu huyo alisema kusogezwa mbele kwa tarehe ya kuanza kwa Ligi Kuu, mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya Simba na Azam, sasa utapangiwa tarehe nyingine ambayo ni wiki moja kabla ya kuanza kwa ligi hiyo.

Akizungumzia suala la ratiba ya ligi hiyo, Osiah alisema nayo inatarajiwa kutangazwa mapema wiki ijayo pamoja na tarehe rasmi ya kuanza kwa ligi hiyo.

Aliongeza kwamba kukamilika kwa mazungumzo hayo ni muhimu kwa kuwa kutasaidia ligi hiyo kuanza bila ya matatizo yoyote kwa klabu zinazoshiriki, TFF na Kamati ya Ligi hasa kutokana na ukweli kuwa baadhi ya mambo yatakayokubaliwa yatalazimika kuingizwa kwenye kanuni za ligi.

Wakati huohuo, Osiah akizungumzia kuhusu chombo kitakachoongoza ligi hiyo alisema TFF ilitoa mapendekezo ya Kamati ya Utendaji kwa Kamati ya Ligi na baadaye kwa viongozi wa klabu za ligi kuhusu muundo wa chombo hicho.

Alisema kulingana na mwongozo wa Katiba ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na Katiba ya TFF, suala hilo kwa sasa linajadiliwa na klabu za Ligi Kuu kwa ajili ya hatua za mwisho.

No comments:

Post a Comment