27 August 2012

Mbinu za kuondokana na msongamano, foleni Dar


Na Mwandishi Wetu

TATIZO la msongamano wa magari katika barabara mbalimbali jijini Dar es Salaam, limekuwa likiongezeka siku hadi siku.

Kwa kawaida, safari ya gari kutoka Mikocheni kwenda katikati ya mji inachukua muda wa dakika 15, lakini hivi sasa safari kama hii yenye umbali wa kilomita 11, hutumia saa moja na nusu au mbili sawa na safari ya kilomita 200 kwenda mkoani Morogoro.

Pamoja na Serikali kuchukua hatua za kumaliza tatizo la usafiri na msongamano wa magari katikati ya jiji hilo, jitihada hizo bado hazijazaa matunda yaliyokusudiwa.

Awali siku za mwisho wa wiki, tatizo la foleni barabarani halikuwa kubwa kama ilivyo sasa.

Ukweli ni kwamba, kero ya msongamano wa magari barabarani ambayo ilizoeleka siku za kazi, hivi sasa huwezi kuitofautisha na siku za mapumziko (wikiendi).

Siku ya Jumamosi ndio mbaya zaidi, tatizo la foleni halina muda maalumu barabarani pengine kutokana na siku hiyo kuwa ya mapumziko, magari mengi huwa barabarani kwa shughuli binafsi.

Kwa wasafiri wanaoshindwa kuvumilia kero za usafiri jijini Dar es Salaam, wamekuwa wakijaribu mbinu mbalimbali za kukwepa foleni kama vile kuondoka nyumbani mapema kuanzia saa 10 usiku ili kuwahi kazini saa mbili asubuhi.

Hayo yote ni kwa ajili ya kukwepa msongamano wa magari na pia kupata uhakika wa usafiri kwa wale wanaotumia usafiri wa umma.

Ifikapo jioni, nyakati za kurudi nyumbani kuna ambao hulazimika kutafuta mahali pa kusubiria mpaka foleni ipungue kabla ya kuendelea na safari zao ingawa wakati mwingine wanaweza kulazimika kusubiri mpaka saa nne usiku.

Uchambuzi huu unaangalia hali ya usafiri na msongamano katikati ya Jiji la Dar es Salaam, chanzo cha tatizo, athari zake, hatua zilizochukuliwa kukabiliana na tatizo hilo, matokeo ya hatua hizi na mwisho ni mapendekezo ya nini cha kufanya.

                 CHANZO CHA KERO YA USAFIRI

Vivutio na shughuli za kiuchumi zilizopo kwenye miji mikubwa ndio kichocheo cha wingi wa watu.

Wingi wa watu hawa husababisha ongezeko la magari na vyombo vingine vya usafiri.

Na kama mji husika haujaweza kujipanga vizuri kukabiliana na ongezeko la watu pamoja na kukidhi mahitaji yao, basi matokeo yake ni mvurugano kama huu wa kero ya usafiri na msongamano mkubwa wa magari unaolikabili jiji la Dar es Salaam ambalo ndio kubwa na maarufu zaidi nchini Tanzania.

Hadhi ya Dar es Salaam imefanya mji huu kuwa ni mahali ambapo panachangia asilimia 80 ya uzalishaji wa nchi, inamaanisha kwamba kuyumba kwa uzalishaji katika eneo hili unaweza kuathiri uchumi wa nchi nzima.

Ni wazi kuwa mipango miji kwa Dar es Salaam bado haijaweza kufikia kiwango kinachostahili kulingana na hadhi na mahitaji yake, kasi ya ongezeko la magari barabarani ni kubwa kuliko uwezo, shughuli nyingi za kibiashara, kiuchumi na kiserikali zimeelekezwa katikati ya mji na pia hali duni ya barabara hususan mitaa inayounganisha barabara kubwa.

Zamani huduma ya usafiri wa umma ilikuwa chini ya mashirika ya umma UDA na KAMATA na yalitumika mabasi makubwa na sio madogo (daladala) ambayo yalikuwa yakibeba watu wengi kwa mara moja na kwa ratiba maalum.

Lakini, tangu kuondoka kwa KAMATA na UDA kushindwa kujiendesha watu binafsi ndio wamekuwa wakiendesha utoaji huduma ya usafiri kwa umma ambapo watu binafsi hawataweza kutokomeza kero ya usafiri peke yao.

Takwimu zilizopo zinaonesha idadi ya mabasi binafsi yanayotoa huduma ya usafiri jijini Dar es Salaam kufikia 6,000 zenye uwezo wa kuhudumia asilimia 43 tu, ya wasafiri waliopo.

Mengine ni kero zinazosababishwa na magari yasiyofuata sheria na taratibu barabarani hivyo kusababisha ajali na hasira.

Kero nyingine huonekana kwa vyombo vya dola ambavyo hushindwa kudhibiti hali ya usafiri na mipango miji inayohitajika kuleta maendeleo hivyo kufanya mji huo kuwa wa kisasa zaidi.

Hizi ni miongoni mwa harakati za kuinua hadhi ya mji wa Dar es Salaam kufikia malengo ya Milenia 2020, ya kuufanya kuwa mji wa kisasa zaidi ikiwa ni pamoja na kukuza uwezo wa wakazi wenye kipato cha chini na kuongeza kipato cha kati kama ilivyo miji mingine mikubwa duniani.

Sababu nyingine za kero ya usafiri na msongamano Dar es Salaam ni pamoja na tabia za madereva za uendeshaji mbovu ikiwemo utamaduni potofu uliojengeka kuwa ni hadhi kumiliki gari.

              Ajali na magari mabovu barabarani

Trafiki, polisi huchukua muda mrefu kufika eneo la tukio na kuyaondoa barabarani magari pindi yanapopata ajali.

Wakazi wa Dar es Salaam kuishi mbali na sehemu zao za kazi kutokana na uhaba wa nyumba za kuishi na zilizopo ni gharama kubwa hivyo hulazimika kutumia muda mrefu na gharama kubwa kwa ajili ya usafiri.

Kuna maeneo mengi yaliyojaa makazi ya watu ambao pia wengi wao wanafanya shughuli zao maeneo yanayofanana (katikati ya mji) hivyo kusababisha msongamano wakiwa wanatoka au kwenda kazini.

Miundombinu iliyopo mingi ni mibovu ikiwa ni pamoja na barabara zenye viwango vya chini (ni ndogo, zina mashimo na hazina uwezo wa kupitisha maji kiasi cha kwamba hata mvua inaponyesha inasababisha foleni).

Hata barabara zilizojengwa hivi karibuni tayari zimeshaanza kuharibika huku shughuli za ujenzi wa barabara zinazofanywa nyakati za matumizi makubwa ya barabara kukosa ubunifu au fursa tofauti za usafiri.

Kwa ushauri au maoni; majira@btl.co.tz, majira2006@yahoo.com. Simu 0719-25 4464 au 077442250, Itaendeea kesho.

No comments:

Post a Comment