Na Said Njuki, Babati
ZAIDI ya wakazi 5,000 wa Vijiji vya Ayamango, Gedamar na Gejedabugh, Wilaya ya Babati, mkoani Manyara, wanadaiwa kutelekezwa na Serikali wakidaiwa kuishi ndani ya eneo la Hifadhi ya Taifa Tarangire, iliyopo chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), kinyume cha sheria kwa zaidi ya miaka 50.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa, wakazi hao wametelekezwa zaidi ya miaka mitano kutokana na makubaliano waliyofikia na Serikali.
Inadaiwa kuwa, katika makubaliano hayo Serikali iliahidi kutowaondoa wakazi hao hadi watakapopatiwa maeneo mbadala lakini hadi sasa, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.
Makubaliano mengine ni wakazi hao kutojishughulisha na shughuli zozote za maendeleo ili kujikimu kimaisha ambapo pamoja na kufikisha malalamiko yao kwa Waziri Mkuu, Bw.Mizengo Pinda, miaka minne iliyopita jitihada zao hazijafanikiwa.
Miaka minne iliyopita, TANAPA ilihakiki mipaka ya hifadhi hiyo na kubaini wakazi hao kuishi ndani ya eneo la hifadhi kinyume cha sheria japo Serikali iliwapa eneo hilo kihalali kwa ajili ya makazi, kilimo na mifugo miaka 40 iliyopita.
Inaelezwa kuwa, vijiji hivyo vilipata baraka zote za usajili ambapo Kijiji cha Gedamar kilipewa namba (AR.KJ.43-1976), Ayamango (AR.KJ.26-1976) na Gejadabugh (AR.KJ.483-1992), kupewa hatimiliki na maeneo yao kutambuliwa kwa ramani.
Kwa mujibu wa barua ya Ofisa Ardhi wilayani humo wakati huo yenye namba BBT/1/vol.11/1477 ya Novemba 10,1988, ambayo ilisainiwa na Bw.Abdallah Tamambele, ilibainisha mipaka halali kati ya hifadhi hiyo na Mamlaka za Ardhi za Vijiji.
Wakati wa Operesheni Vijiji vya Ujamaa, wananchi wengi kutoka maeneo mbalimbali wilayani Babati ambao hawakuwa na maeneo ya kilimo, inadaiwa walipatiwa maeneo katika vijiji hivyo.
Kutokana na Hifadhi ya Tarangire kuhakiki mpaka wake, matokeo hayo yalizua mtafaruku mkubwa baada ya kubainika eneo lenye ekari 16,249, lipo ndani ya vijiji vya wakazi hao ambao walitakiwa kuondoka mara moja na kusitisha matumizi ya ardhi.
Hali hiyo iliwafanya wananchi kukimbilia mahakamani kupinga agizo hilo na baadaye kukaa pamoja kati ya Serikali, uongozi wa hifadhi na hatimaye kuamriwa TANAPA iwalipe fidia.
Makubaliano hayo yalitekelezwa lakini Serikali ilijitwisha mzigo wa kuwatafutia wakazi hao eneo mbadala la kuishi kabla hawajaondoka, ahadi ambayo haijatekelezwa hadi sasa.
Hata hivyo, watumishi wa hifadhi hiyo wanadaiwa kuwashinikiza wananchi hao kuondoka kwa nguvu bila kuzingatia makubaliano.
Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Bw.Dismas Nakei, aliwahi kumwandikia barua Waziri Mkuu, Bw.Pinda yenye namba MB/BBT-V/2008/15 ya mwaka 2008, akimlalamikia kuwa wananchi wa vijiji hivyo wapo katika baa la njaa kwa vipindi vitatu mfululizo kutokana na mgogoro wa muda mrefu hivyo kuzuiwa kulima na kufuga.
“Hali hii inawafanya wananchi wakose chakula na sasa wana njaa, pia wananyeshewa na mvua ndani ya nyumba zao ambazo zimechakaa kwa kukosa matengenezo baada ya kuzuiwa kuziendeleza.
“Kwa muda mrefu sasa hawawezi kuchimba hata choo kwani hawana ruhusa ya kufanya hivyo licha ya umuhimu wa kuwa navyo kwa afya zao,” ilieleza sehemu ya barua hiyo.
Bw.Nakei alimwomba Waziri Mkuu, Bw.Pinda kumaliza utata huo na kusisitiza kuwa, wakati ufumbuzi wake ukiendelea wananchi waruhusiwe kulima na kufuga ili kujikinga na baa la njaa.
Pia Bw.Nakei alitaka wananchi hao waruhusiwe kukarabati nyumba zao na kuchimba vyoo kwa faida yao na taifa kwa ujumla lakini hakuna lililotekelezwa hadi sasa.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw.Khalidi Mandia, alikiri kuwepo tatizo hilo na kulijua kabla hajahamia wilayani humo kwa sababu walikuwa wakilizungumza katika vikao vya Kamati ya Ulinzi na Usalama.
“Tatizo hili la muda mrefu lakini nikuhakikishie kuwa, tunajiandaa kulitafutia ufumbuzi wa kudumu, tulikwamishwa na baadhi ya majukumu ya kitaifa lakini hivi sasa tupo kwenye nafasi nzuri ya kulishughulikia,” alisema Bw.Mandia.
No comments:
Post a Comment