24 August 2012

Machinga Complex wamjibu Masaburi



Na Zourha Malisa

BODI ya Wakurugenzi Jengo la Machinga Complex, imeshtushwa na taarifa iliyotolewa na Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dkt. Didas Masaburi, kuwa Jiji hilo linakusudia kumuomba Rais Jakaya Kikwete, aruhusu jengo hilo lichukuliwe na Serikali.


Katika maelezo yake, Dkt. Masaburi alisema hatua hiyo itawezesha jengo hilo kuendeshwa kiushindani na kuruhusu wafanyabishara wabungwa wapangishe tofauti na ilivyo sasa.

Mwenyekiti wa Bodi hiyo Bw. Godwin Mbande, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na Majira juu ya kauli aliyoitoa Dkt. Masaburi kuwa, Jiji la Dar es Salaam liko hoi kifedha na halina uwezo wa kulipa mkopo wa sh. bilioni 32, walizokopa Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ili kujenga jengo hilo.

Katika maelezo yake kama alivyonukuliwa na gazeti moja (sio Majira), Dkt. Masaburi, alisema Jiji hilo linaangalia uwezekano kuiruhusu NSSF kulipiga jengo hilo mnada ili kupata fedha zake.

Bw. Mbande alisema, hawajawahi kukaa na Dkt. Masaburi ili kuzungumzia suala la jengo hilo kupigwa mnada na hakuna sababu yoyote ya kufanya hivyo kama anavyodai.

“Hakuna sababu ya kupiga mnada jengo hili, jambo la msingi ni kupanga mikakati na kuangalia uwezekano wa kuwawezesha wafanyabiashara wadogo ili wafanye biashara zao,” alisema.

Aliongeza kuwa, suala la malimbikizo ya deni, Bodi hiyo tayari ilikutana na kutoa taarifa kwa viongozi juu ya nini kinatakiwa kufanyika lakini si kulipiga mnada.

“Bodi ina mikakati ya kuliboresha jengo hili kwa kuanzisha gulio hivi karibuni na wafanyabiashara kutapata fursa ya kuuza bidhaa zao kwa njia ya mnada,” alisema Bw. Mbande na kusisitiza kuwa, hicho ndicho anachofahamu yeye ambapo gulio hilo litafanyika mara mbili katika wiki.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa soko hilo, Bw. Abubakari Rakesh, naye alidai kushangazwa na kauli aliyoitoa Dkt. Masaburi na kuongeza kuwa, wamepanga kukutana Jumamosi na kutoa tamko.

“Nimeshangazwa na kauli ya Meya wa Jiji, hivi sasa sipo tayari kuzungumzia jambo hili hadi tutakapokaa kikao chetu na kutoa tamko la pamoja,” alisema Bw. Rakesh.

1 comment:

  1. Masaburi na wenzake wasitake kukwepa wajibu kwa kuhamisha tatizo serikali kuu. Tatizo linatokana na uamuzi mbovu wa kusudi ili mradi kuna ulaji.Walifanya uamuzi wa kujenga machinga complex kwa kujidai ni uwekezaji sahihi huku wakijua nia yao ni kutoa kandarasi ya ujenzi ili waweke cha juu na kujipatia ulaji. Hivi watu kama hawa watabebwa hadi lini na serikali ya CCM? Hakuna kitu kama machinga kwenye complex kama ile wakati machinga halisi wanaranda kuizunguka.

    ReplyDelete