30 August 2012
Kocha Yanga kuwekwa kiti moto
Na Zahoro Mlanzi
SIKU moja baada ya Kocha Mkuu wa timu ya Yanga, Tom Saintfeit kudaiwa kusema hajatimiziwa baadhi ya vitu katika mkataba wake na kutishia kuondoka, uongozi wa Yanga umekuja juu na kusema utamchunguza kocha huyo kutokakana na kauli alizozitoa kama ni za kweli na kisha kuangalia vitu gani ambavyo hawajamtimizia.
Mbali na hilo, timu hiyo imevunja ukimya juu ya ujio wa beki wao mpya kutoka Rwanda, Mbuyu Twite kwa kusema atatua nchini leo mchana na wanatarajia atapata mapokezi ya aina yake kutokana na mengi yanayozungumzwa juu yake.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa timu hiyo, Louis Sendeu baada ya kuulizwa madai ya kocha huyo kwamba hawajamtimiza mambo yake ya msingi, alisema watakachofanya kwa sasa ni kuzungumza naye kama kweli ametoa kauli hizo na baada ya kubaini ukweli watajua nini cha kufanya.
"Ni kweli tumesikia amezungumza na chombo kimoja cha habari akidai kuna vitu katika mkataba wake hajatimiziwa, lakini kama uongozi wa Yanga hizo taarifa tunazifanyia kazi kwa kukaa naye ili tujue kama kweli amezungumza au laa.
"Tutafanya uchunguzi juu ya hilo na kisha kuangalia kama kweli kuna mambo hatujatimiza katika makubaliono yetu tuliyoingia na kocha Saintfeit na baada ya hapo tutajua la kufanya, lakini tumesikitishwa na taarifa hizo," alisema Sendeu
Alisema katika mkataba huo, kocha anapaswa atimize anayopaswa kutimiza na kwa upande wa uongozi pia utahakikisha kwa asilimia zote unatimiza yanayotakiwa.
Katika hatua nyingine, timu hiyo imesema Jumamosi itashuka uwanjani kuumana na Coastal Union ya Tanga kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo imetamba wachezaji wake wote iliyowasajili msimu huu itawatumia katika mchezo huo.
Alisema katika mchezo huo kiiingilio ni sh. 20,000 kwa Viti Maalumu A (VIP A), VIP B na C ni sh. 10,000, viti vya machungwa ni sh. 5,000 na viti vya kijani na bluu ni sh. 3,000 ambapo wanawaomba mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi.
Sendeu alisema timu hiyo leo iitatembelea Kampuni ya Bia ya Tanzania (TBL), ambao ndiyo wadhamini wao kupitia bia ya Kilimanjaro ambapo watakwenda kujifunza jinsi bia hiyo inavyotengezwa na mambo mengine.
Mbali na hilo, pia alizungumzia ujio wa Twite ambapo alisema beki huyo atatua nchini leo saa 9, alasiri na anawaomba mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kumpokea.
Alisema wanajua wapinzani wao Simba, walidai wana RB ya kumkamata beki huyo, lakini wao hawatishwi na maneno hayo kwani wamemsajili kwa kufuata taratibu zote na kwamba ni mchezaji wao halali.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment