29 August 2012

JK aomboleza vifo vya askari watatu JWTZ


Na Mwandishi Wetu

AMIRI Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Jakaya  Kikwete, ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Davis Mwamunyange, kuomboleza vifo vya askari watatu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliokuwa wanalinda amani Darfur, nchini Sudan, ambavyo vimetokea mwishoni mwa wiki iliyopita.


Taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, ilisema Rais Kikwete amepokea taarifa hiyo kwa mshtuko na huzuni kubwa.

Alisema vifo vya vijana hao vinasikitisha zaidi hasa kwa kuzingatia kuwa wamepoteza maisha katika utumishi muhimu wa nchi yetu wakati wakilinda amani ya Bara la Afrika.

“Tutaendelea kuwakumbuka kwa utumishi uliotukuka, mchango wao kwa nchi yetu na Bara la Afrika, kutokana na vifo hivi natumia salamu za rambirambi kupitia kwako.

“Naomba uniwasilishie pole zangu nyingi kwa familia za vijana wetu ukiwajulisha kuwa, moyo wangu uko nao wakati wa kipindi hiki kigumu cha kuwapoteza wapendwa wao,” alisema.

Naungana nao kumwomba Mungu, Mwingi wa Rehema, aziweke pema peponi roho za marehemu.”

Rais Kikwete pia alimtaka Jenerali Mwamunyange kuwafikishia salamu za pole makamanda na askari wote nchini ambao wanaolinda amani Darfur, askari hawa ni sehemu ya wanajeshi 850 wa Tanzania waliopo nchini humo na mwenzao mmoja ambaye hajulikani alipo hadi sasa baada ya kupoteza maisha katika ajali ya gari ambalo lilisombwa na maji wakati wakivuka mto kwenye Kijiji cha Hamada, eneo la Manawasha.


1 comment:

  1. Tunaungana na Mheshimiwa Raisi Jakaya Mrisho Kikwete kwa kutoa salamu za rambirambi kwa
    familia za wanajeshi hao wanne waliopoteza maisha huku Durful Sudani wakilinda amani

    Tanzania kama tunavyojua ni kati ya nchi ambazo zimepigania kupata amani/kuleta uhuru
    kusini mwa bara la Afrika hususani Msumbiji ,Rhodesia/Zimbabwe , Angola. na hata
    Afrika kusini hadi nchi hizo kupata uhuru wake wa kweli.

    Mbali na mapigano hayo ya kuwezesha kusini mwa Afrika kupata Uhuru pia tumekuwa tunashiriki
    kulinda amani kwenye baadhi ya nchi barani Afrika , na Ulaya pia kama tunavyoona nchini Sudani
    sasa kuna nchi ya Sudani ya Kaskazini na Sudani na Sudani ya Kusini ikiwa ni juhudi za umoja wa
    Mataifa ikiwemo Tanzania kuzitenganisha ili kuleta amani.

    Ni wakati sasa umefika viongozi wetu hasa tukianzia na Mheshimiwa Raisi Jakaya Kikwete
    kuzungumzia amani ili itekelezwe kwa vitendo kwa nguvu zote na viongozi wengine hususani
    maraisi wa nchi zao ili nao waige mfano wa Tanzania kwa kuleta amani barani Afrika.

    Kama inavyoonekana amani hutoweka pale ubinafsi unapotawala , nchi kama Sudani kuna utajiri
    mkubwa wa mafuta hivyo ubinafsi /uchoyo wa baadhi ya viongozi unasababisha amani itoweke,
    kwa sababu siyo mrefu uliopita karibu nchi hizi ambazo ilkuwamoja karibu iingie kwenye vita
    kwa ajili ya kipande cha nchi ambacho kinaaminika kina mafuta mengi, hadi mgogoro huo
    uliposuluhishwa na waziri wa mambo ya nje wa marekani

    Tuangalie huko Kongo kwenye utajiri wa madini amani inakosekana kwa sababu hizohizo
    Mauaji yaliyotokea huko Afrika kusini kwenye machimbo ya dhahabu na kuuwa watu 34
    ni sehemu ya uchoyo wa kutokugawana vema mali asili hizi

    Nchi nyingi zimeingia kwenye migogoro ya wenyewe kwa wenyewe kwa sababu wa utajiri wa
    aidha madini , mafuta nk na kutokana na hali hiyo watu wengi wasiokuwa na hatia wamepoteza maisha
    yao kwenye mapigano hayo

    Aidha napenda kumpongeza Mheshimiwa Raisi kwa hatua za kuzima moto wa mgogoro
    wa ziwa nyasa na kumwita/ kumwalika Raisi wa Malawi ili kuleta amani kwenye nchi hizi
    mbili kutokana na chokochoko za Malawi kudai ziwa Nyasa ni lao na kuanza kuruhusu
    kampuni za kigeni kutafuta mafuta na gesi.

    Watanzania tuendelee kulinda amani tuliyonayo kwani ni vigumu kuirudisha ikipotea kama
    neno la Mungu linavyosema " Tafuteni kuwa na Amani na watu wote"Waebrania 12:14
    Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika na watu wake

    ReplyDelete