07 August 2012

Kesi ya akina Hassanoo yapigwa kalenda


Na Rehema Mohamed

UPANDE wa Mashtaka katika kesi ya wizi wa madini aina ya shaba yenye thamani ya zaidi ya sh.milioni 400 umebadili hati ya mashtaka ya kesi hiyo pamoja na kuwasomea upya mashtaka yanayowakabili washtakiwa wa kesi hiyo.


Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) Hassan Hasaan 'Hasanoo',Wambura Mahega na Dkt.Najim Msenga.

Wakili wa serikali Teophil Mutakyao alidai katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Devota Kisoka alitoa ombi la kufanya mabadiliko ya hati hiyo ya mashtaka wakati kesi hiyo ilipoletwa kwa ajili ya kusikilizwa.

Mutakyao alidai kuwa lengo la kufanya mabadiliko ni kuweka vizuri vifungu vya sheria katika hati hiyo pamoja na kuweka vizuri thamani halisi ya mali iliyoibiwa.

Akiwasomea upya mashtaka yao ,wakili Mutakyao alidai kuwa katika kosa la kwanza washtakiwa hao wanadaiwa Agosti 26 ,2011 walikula njama ya kutenda kosa la wizi eneo la Bahari Beach ,Kinondoni.

Katika shtaka la pili alidaiwa kuwa Agosti 26,2011 eneo la Bahari Beach washtakiwa hao waliiba tani 26.475 za madini aina ya shaba yenye thamani ya sh.milioni 333,467,848.13 mali ya kampuni ya Libarty Express Tanzania Ltd yakisafirishwa kutoka nchini Zambia .

Kosa la tatu washtakiwa hao wanadaiwa kuwa katika tarehe hiyo walipokea kiasi hicho cha shaba wakati wakijua mali hiyo ya wizi.

Washtakiwa wote walikana kutenda makosa hayo ambapo wakili wa utetezi aliyejitambulisha kwa jina  la Mark aliomba kesi hiyo iahirishwe ili aweze kuwasiliana na mawakili wenzake kabla kesi hiyo haijaanza kusikilizwa.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 6, mwaka huu itakapoletwa kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.

No comments:

Post a Comment