07 August 2012
SMT yawapa changamoto wanamuziki nchini
Na Mwali Ibrahim
SHIRIKISHO la Muziki Tanzania (SMT) limewataka wanamuziki kutunga nyimbo zinazohusu utamaduni wa Mtanzania ili kuutangaza vizuri nje ya nchi.
Akizungumza Dar es Salaam jana Katibu Mkuu wa SMT Salim Omari Mwinyi, wakati wa mapokezi ya bendi ya muziki wa dansi ya Extra Bongo iliyokuwa kwenye ziara ya mwezi mmoja nchini Finland katika tamasha la First Africa ili kuutangaza utamaduni wa Kitanzania haina budi wanamuziki kutunga nyimbo za utamaduni wetu.
Alisema, hiyo ni changamoto kubwa kwa wanamuziki wa hapa nchini, kama wanataka kuzitangaza kazi zao Kimataifa na hata kupata nafasi ya kuweza kutoa burudani katika majukwaa makubwa.
"Ziara ya Extra bongo iwe changamoto kwa wanamuziki wengine kutunga nyimbo zinazobeba utamaduni wetu kwani mashabiki wa nje wanapenda aina hiyo ya muziki na sisi kama Shirikisho tutasimamia katika hilo," alisema.
Akizungumzia ziara yao Mkurugenzi wa bendi hiyo Ally Choki alisema, ni ziara iliyokuwa na mafanikio makubwa na wameweza kutengeneza video ya wimbo wa Ufisadi wa mapenzi huku wakishirikiana na wanamuziki wa Finland.
"Kuna wanafunzi ambao alikuwa akiwafundisha Nyamwela katika vyuo mbalimbali vya nchini humo, ambapo alipata nafasi ya kuvifundisha na tumewatumia katika kuongeza chachu katika video hii," alisema.
Aliongeza kuwa baada ya kufanya uzinduzi wa albamu yao ya Mtenda akitendewa nchini humo, pia alipanga kuizindua tena nchini Septemba , lakini wameamua kusogeza mbele ili kuweza kuhakikisha wanamaliza kutengeneza video ya nyimb hizo kwanza.
Kwa upande wake Nyamwela alisema, alipata nafasi kubwa ya kufundisha muziki katika vyuo vikuu sita vya muziki nchini humo, ambapo ilikuwa ni sehemu ya pili ya mkataba wake ambapo awali alishawafundisha na safari hii alikuwa anamalizia.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment