21 August 2012

Kanisa latoa msaada wa baiskeli kwa walemavu


Na Stella Aron

WITO umetolewa kwa Watanzania kuona umuhimu wa kuwasaidia watu wenye ulemavu hasa wa miguu kwa kuwapa baiskeli ili wazitumie kufika maeneo mbalimbali ya huduma za msingi.

Askofu wa Kanisa la Christin Mission Fellowship, Mgulu Kilimba, aliyasema hayo Dar es Salaam juzi wakati akikabidhi msaada wa baiskeli kwa watu wenye ulemavu.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Bw. Jordan Rugimbana ambapo Askofu Kilimba aliongeza kuwa, idadi kubwa ya watu wenye ulemavu wa miguu, hutembea kwa tabu na kusababisha washindwe kufika katika maeneo mengi ya huduma.

“Ili kupunguza tatizo hili, Watanzania wote tunapaswa kushirikiana na kuwasaidia wenzetu, baadhi yao wafanyabiashara na wanafunzi ambao kipindi cha mvua hupata tabu sana,” alisema.

Aliongeza kuwa, kwa kutambua umuhimu wa kulisaidia kundi hilo, Kanisa limetoa msaada wa baiskeli 26 zenye thamani ya sh. milioni 20 kwa watu wenye ulemavu wa miguu wanaioshi jijini Dar es Salaam na Mtwara.

Askofu Kilimba alisema lengo lao ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2020, watu wenye ulemavu wa viungo wanakwenda shule na watu wazima wanafanya shughuli zao kama kawaida.

“Kanisa letu lina lengo la kuwafikia watu milioni mbili ambao wan ulemavu wa viungo hadi kufikia mwaka 2020, kazi ya utoaji misaada ilianza mwaka 2006.

“Hadi sasa tayari tumesaidia watu 5,000 wenye ulemavu kwa kuwawezesha kutoka sehemu moja kwenda nyingine wakitumia baiskeli badala ya kuburuzika kwa mikono na makalio,” alisema.

Akitoa neno la shukrani kwa msaada huo, mwanafunzi wa darasa la saba katika shule ya Jeshi la Wokovu Dar es Salaam, Abel John, alisema baiskeli hiyo itamsaidia kwenda shule, kurudi pamoja na kupunguza kero mbalimbali alizokuwa akizipata.

Kwa upande wake, Bw. Rugimbana alilishukuru kanisa kwa kutoa msaada huo na kuwaomba watu binafsi, taasisi na mashirika mbalimbali kuiga mfano huo.

No comments:

Post a Comment