27 August 2012

Gharama elekezi za Sekta ya Ulinzi Binafsi


Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha Sekta ya Ulinzi Binafsi nchini (TSIA), kimetangaza viwango vipya vya gharama elekezi kwa shughuli za ulinzi wa kampuni binafsi zinazotumia kiwango cha mshahara sh.80,000.

Viwango hivyo vitalipwa kila mwezi kwa kila mlinzi mmoja ambapo wateja wanaotumia ulinzi binafsi, watatakiwa kuvilipa.

Wiki iliyopita, gazeti hili liliandika kwa makosa habari iliyohusu
kupanda kwa gharama za mishahara ya walinzi wa kampuni binafsi badala ya viwango elekezi hivyo kusababisha usumbufu mkubwa kwa wadau wa sekta hiyo na uongozi wa TSIA.

Usahihi wa taarifa ambayo ilitolewa na Mwenyekiti wa TSIA, Bw.Almas Maige, alisema chama hicho kimeunga mkono viwango vilivyotangazwa katika zabuni za shughuli za ulinzi binafsi na Wakala wa Manunuzi Serikalini (GPSA).

Bw.Maige alisema viwango hivyo vya GPSA ndiyo vya chini kabisa kwani vinalingana na gharama halisi za mlinzi mmoja mmoja dhidi ya mdau mwenye Kampuni ya Ulinzi kwa mshahara wa mlinzi sh. 80,000 kwa mwezi.

Viwango elekezi vitaziwezesha kampuni za ulinzi binafsi kulipa kodi zote za Serikali, ikiwemo ya Ongezeko la Thamani (VAT), SDL, sare za walinzi, likizo zao na malipo ya Mifuko ya Hifadhi za Jamii.

Alisema Agosti 14, mwaka huu, GPSA walitoa barua ya gharama elekezi kwa shughuli za ulinzi ambazo zitalipwa na Serikali pamoja na Mashirika ya Umma inayosema kuanzia sasa, gharama za huduma za ulinzi wenye silaha ni sh.280,000, kwa mwezi.

Gharama ya ulinzi bila silaha sh. 220,000 kwa mwezi, gharama ya usimamizi sh. 200,000 kwa mwezi na usindikizaji fedha au mali kwa safari moja sh. 20,000.

Alisema gharama ya usindikizaji bila silaha kwa safari moja itabaki
sh. 60,000 na usindikizaji wenye silaha utakuwa sh. 80,000.

Bw.Maige aliongeza kuwa, mchanganuo wa gharama za mlinzi mmoja kwa kampuni ni mshahara wa mlinzi mmoja sh. 80,000 kwa mwezi, likizo sh. 6,666.66 na saa za ziada kwa mwezi sh. 63,999 ambapo asilimia 10 yake, itapelekwa mifuko ya NSSF na PPF, kwa mwezi ambayo itakuwa sh. 14,399.90.

Pesa ya kufanya kazi katika mazingira magumu kwa mwezi sh. 23,999,83, sare kwa mwezi sh. 12,500, asilimia sita ni tozo ya SDL sh. 8,639,94 kwa mwezi ambapo jumla ya gharama zote za kampuni kwa kila mlinzi ni sh. 210,405,33 kwa mwezi.

Aliongeza kuwa, gharama hizo si malipo kwa walinzi bali kwa kampuni za ulinzi na kusisitiza kuwa, hakuna mishahara ya walinzi iliyopandishwa kama tulivyoripoti katika gazeti hili.

Kwa ufafanuzi zaidi kuhusu habari hii, TSIA imetoa tangazo katika
gazeti hili ukurasa wa pili.Mhariri anaomba radhi kwa usumbufu wowote uliojitokeza kwa wasomaji pamoja na wadau.





No comments:

Post a Comment